FEDHA ZA BOOST ZALETA MAGEUZI MAKUBWA HANDENI MJI

Na Mwandishi Wetu, Handeni TC

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Mji Handeni kwa lengo la kujifunza utekelezaji wa Mradi wa BOOST unaolenga kuboresha miundombinu ya elimu ya msingi na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Mradi wa BOOST kutoka Jiji la Tanga ilitembelea miradi miwili mikubwa ya ujenzi wa shule za msingi inayotekelezwa na Halmashauri ya Mji Handeni.

Miradi hiyo ni ujenzi wa Shule ya Msingi Kwediziwa uliogharimu Sh milioni 540.3, ambapo madarasa 16 pamoja na matundu 28 ya vyoo yalijengwa, na Shule ya Msingi Mdoe, ambako Sh. milioni 543 zimetumika kujenga madarasa 14 na matundu 28 ya vyoo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Handeni na Mratibu wa Mradi wa BOOST, Elizabeth Mwakalonge, amesema utekelezaji wa mradi huo umeleta mafanikio makubwa ikiwamo kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, kupunguza umbali wanaotembea wanafunzi kufuata shule pamoja na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu Jiji la Tanga na Mjumbe wa Kamati ya Mradi wa BOOST, Kurwa Mhoja, amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza uzoefu wa utekelezaji wa mradi wa BOOST katika Halmashauri ya Mji Handeni pamoja na kubadilishana uzoefu na maafisa elimu ili kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo katika Jiji la Tanga.

Ameongeza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

0/Post a Comment/Comments