:::::::
Ashrack Miraji
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Idd Mfinanga, akiambatana na baadhi ya madiwani, amewasili katika Ofisi ya Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mhe. John Mapato Meela, kwa lengo la kumpongeza na kujitambulisha rasmi.
Ziara hiyo imefanyika leo, ikiwa ni siku ya kwanza kwa Meela kuanza rasmi majukumu yake baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo. Meela ameahidi kuwatumikia wananchi wote wa Halmashauri ya Moshi bila upendeleo, huku akisisitiza dhamira ya kuimarisha utendaji na uwajibikaji.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mbunge wa Vunjo na wananchi wa jimbo hilo, Mfinanga alimpongeza Meela kwa kuchaguliwa na kuahidi ushirikiano wa karibu kati ya ofisi ya mbunge na uongozi wa Halmashauri, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Mfinanga alisisitiza kuwa Jimbo la Vunjo limejipanga kushirikiana na Halmashauri bega kwa bega ili kuharakisha maendeleo, huku akibainisha kuwa ushirikiano huo utakuwa nguzo muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Post a Comment