.....................
GEITA
SERIKALI mkoani Geita imewataka wataalamu wa kilimo kuondoka maofsini ili kuwatembelea na kuwashauri wakulima namna bora ya kulima, kupanda na kuvuna kwa tija.
Hatua hiyo inakusudiwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuinua uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema hayo wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa kilimo kutoka wilaya tano za mkoa huo huku akisisitiza maofisa ugani kuwafikia wakulima mashambani katika kipindi hiki cha kilimo.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika kilimo kutokana na ukweli kwamba zaidi ya aslimia 80 ya watanzania wanajihusisha na kilimo na kwamba ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda ni muhimu sana kuwa na mali ghafi zitokanazo na kilimo.
Kutokana na hali hiyo, Shigela amewahimiza wakulima kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia chakula cha kutosha na kubaki na ziada ya kuuza na kujipatia pesa.
Kwa upande wake kaimu Katibu tawala mkoa wa Geita, Dkt Elfasi Msenya, amedai serikali kwa kutambua umuhimu wa kilimo wamelazimika kuwakusanya wakulima wa mazao mbalimbali ili kuwajengea uwezo kwa lengo la kuzalisha kwa tija.
Baadhi ya makundi yaliyofikiwa na elimu ya uzalishaji bora wa mazao ni pamoja na wakuu wa wilaya za mkoa huo, wakurugenzi wa halmashauri, maofisa kilimo wilaya, wanachama wa vyama vya ushirika,wauza pembejeo pamoja na wakulima 40 kutoka kila wilaya.
Mkurugenzi msaidizi Idara ya maendeleo ya mazao kutoka Wizara ya kilimo, Samson Mponeja, amewataka wakulima kubadilika ki fikra kwa kuzingatia namna bora ya kilimo cha kisasa badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea.
Amesema awali ardhi iliyokuwa ikitumika kwa shughuli za kilimo inaendelea kupungua kutokana na ongezeko la watu na makazi, hivyo ipo haja kubwa ya wakulima kuzingatia maelekezo ya wataalamu katika kilimo.
Amesema njia bora ya kuzalisha kwa tija ni kuanza tathimini ya afya ya udongo, kuchagua mbegu bora kulingana na hali ya hewa ya maeneo husika, kupanda kwa maelekezo, mbolea, palizi pamoja na kuvuna kwa usahihi.
Kikao cha wadau wa mazao ya Choroko,Dengu, Mbaazi na Alizeti mkoani Geita kimeongozwa na Tathimini ya utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala msimu wa 2024/25 na maandalizi ya msimu wa 2025/26.
Mwisho.



Post a Comment