Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe,akizungumza na wanachama wa Saccos ya walimu Chato
Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe, akiwa na Mwl. wake Mathias Laurian(kulia) wakiwa katika picha ya pamoja.

............
CHATO
MBUNGE wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe, amemtambulisha mwalimu wake aliyemfundisha shule ya msingi Rutunguru Muganza baada ya kukutana kwenye mkutano mkuu wa Chama Cha kuweka na kukopa cha walimu Chato(Chato Teachers Saccos).
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa uvumi wa baadhi ya watu wakidai Mbunge huyo siyo mzaliwa wa Jimbo la Chato Kaskazini.
Kutokana na hali hiyo, Magembe amelazimika kuuthibitishia umma wa Chato kuwa yeye ni mzaliwa halisi wa wilaya hiyo kwa kumtambulisha mwalimu wake aliyemfundisha shule ya msingi mwaka 1986.
Hata hivyo katika mkutano huo, ambao Mbunge huyo alikuwa mgeni rasmi, ameonyesha kuvutiwa na usimamizi mzuri wa Saccos hiyo na kulazimika kununua hisa za takribani shilingi 1,000,000 ili kuwa mwanachama mpya na aliye hai.
Mbali na hilo, Mbunge huyo amelazimika kutatua changamoto ya usafiri kwa watumishi wa Saccos hiyo baada ya kutoa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 2 kati ya milioni 2.6 zinazohitajika kwaajili ya ununuzi wa pikipiki ya taasisi hiyo.
Kadhalika amewataka viongozi wa taasisi hiyo kushirikiana katika uendeshaji wa taasisi hiyo, kuwa wawazi katika fedha za wanachama pamoja kubuni vyanzo vingine vya kuyaongezea fedha.
Kwa upande wake Mwalimu aliyemfundisha Mbunge huyo, Mathias Rweyendera Laurian, amempongeza Magembe kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini huku akimwombea mafanikio katika utumishi wake.
Amesema Mbunge huyo amekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Rutunguru tangu mwaka 1981 hadi mwaka 1987 alipohitimu na kwenda elimu ya Sekondari, huku akidai kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mwenye nidhamu na bidii katika masomo yake.
Katika mkutano huo, Mrajis msaidizi wa Ushirika mkoa wa Geita, Doreen Mwanri, amesema Chama Cha Saccos ya walimu chato kiefanikiwa kununua hisa nyingi kwenye Benk mpya ya ushirika nchini, na kwamba kimeonekana kujiendesha kwa faida na kushika nafasi ya pili katika mkoa huo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama hicho, Mwl. Pius Katani, amemshukuru sana Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuguswa na uendeshaji wa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja kuamua kuwanunulia pikikipiki kama nyenzo ya kurahisisha usafiri kwa watumishi hao.
Mwenyekiti wa Saccos hiyo, Mwl. Petro Rwegasira ametumia fursa hiyo kuwahimiza walimu na watumishi wengine wa umma kuendelea kujiunga na Saccos hiyo ili kupunguza fedheha na uzalilishaji unaofanywa kwa watumishi wa umma na taasisi binafsi za fedha.
Mwisho.



Post a Comment