MBUNGE LUTANDULA KUZIKA ZIMWI LILILOKUNYWA DAMU ZA WATOTO 18


 . ....

CHATO

HATIMAYE Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini, Pascal Lukas Lutandula, ameamua kupambana na zimwi la vifo vya wanafunzi wa shule ya msingi Ibondo ambao awali walikuwa wakipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wanafunzi takribani 18 wamepoteza maisha wakati wakivuka barabara kuu ya Bwanga kwenda Mwanza, wakati wakivuka kutoka Kijiji cha Ibondo "B" ili kwenda kusoma kwenye shule ya msingi Ibondo "A".

Hatua hiyo imekuwa ikisababisha majonzi, maumivu na hasara kubwa ya nguvu kazi ya baadaye licha ya wananchi kukosa namna bora ya kuepukana na ajali hizo.

Katika kudhibiti vifo hivyo, Lutandula, amelazimika kutumia fedha zake binafsi takribani milioni 4 kwaajili ya kununua mbao, misumari, huku akiahidi kuendelea kugharamia malipo ya mafundi watakao paua na kuezeka vyumba viwili vya madarasa pamoja na Ofisi moja ya walimu kwenye shule shikizi ya Ibondo "B".

Baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa shule hiyo, amesema akiwa kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Chato kusini Bungeni, hawezi kuendelea kuona vifo vya wananchi wake vikiendelea pasipo kuwa na suluhisho la kudumu.

"Kutokana na adha ya vifo vingi vya wananchi, binafsi ninaungana na ninyi kuhakikisha shule hii inakamilika haraka ili kuanzia Januari 2026 watoto wasilazimike kwenda kusoma shule ya Ibondo A badala yake wasomee hapa hapa".

"Ndiyo maana nimelazimika kununua mbao zote za kupaulia vyumba hivi ambavyo mlijenga kwa nguvu zenu wenyewe na kukwama kwenye suala la kuezeka, niwahakikishie na gharama za mafundi nitazilipa mimi mwenyewe ili ibaki kazi ya kuchimba vyoo angalau matundu nane" amesema Lutandula.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ibondo B, Phaustine Malunde, amempongeza Mbunge kwa kuguswa na kadhia ya muda mrefu ya wanafunzi kutembea umbali mrefu pamoja na vifo vinavyoweza kuepukika.

Kitendo cha Mbunge kuhakikisha shule hiyo inakamilika na Wanafunzi kuanza kupata masomo katika eneo hilo, ni sawa na kuzika zimwi lililokuwa likinyonya damu za wanafunzi kwa muda mrefu.

                        Mwisho.

0/Post a Comment/Comments