ROSTAM, TCCIA WAFUNGUA MLANGO MPYA WA MAGEUZI YA BIASHARA NCHINI

::::::::

Wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji kutoka sekta mbalimbali nchini wanatarajia kunufaika na maboresho mapya ya mazingira ya biashara yanayoandaliwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Maboresho hayo yanatajwa kuchochewa na mazungumzo ya kimkakati kati ya Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, na mfanyabiashara maarufu nchini, Bw. Rostam Aziz.

Katika mazungumzo hayo, wawili hao waliweka mbele maslahi ya wanachama wa TCCIA na wafanyabiashara kwa ujumla, wakisisitiza haja ya kuwa na chemba imara, inayoaminiwa na inayosikika katika mchakato wa kutengeneza sera rafiki kwa biashara.



Bw. Rostam Aziz alisema chemba madhubuti ndiyo msingi wa ustawi wa wafanyabiashara na uchumi wa Taifa.
“Chemba ni chombo muhimu kwa ukuaji wa biashara. Inahitaji sapoti kutoka kwa wafanyabiashara na hata kwa Rais wa nchi. Tukijenga Chemba imara, tunajenga Tanzania yenye uchumi thabiti. Huu ni wakati wa kuanza ukurasa mpya,” alisema.

Akaongeza kuwa Watanzania wana wajibu wa kutambua mchango wa wafanyabiashara wazawa katika kukuza uchumi.
“Mimi nilipopitia changamoto, Chemba ilinilinda. Wafanyabiashara wakiona jinsi inavyotetea maslahi yao, wataelewa thamani yake. Ni wakati wa kuunga mkono jitihada za wazawa badala ya kuwanyooshea vidole,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, alisema mafanikio ya Chemba hayawezi kutenganishwa na mafanikio ya wanachama wake.
“Chemba ikifanya vizuri, kila mfanyabiashara atanufaika. Tunahitaji kuijenga upya, kuipa nguvu na kuhakikisha sauti yetu inasikika kwenye majukwaa ya sera. Tukisimama kama mtu mmoja, changamoto nyingi zitatatuliwa kwa ufanisi,” alisema Minja.

Mazungumzo hayo yametoa dira mpya ya ushirikiano kati ya TCCIA na wadau wakubwa wa sekta binafsi, lengo likiwa ni kujenga chemba jumuishi, imara na yenye uwezo wa kuongoza mageuzi chanya katika mfumo wa biashara na uwekezaji nchini.





**Mwisho**
 

0/Post a Comment/Comments