::::::
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kufanya tathmini ya kutanua barabara katika mpaka wa Tunduma unaopitisha magari yaendayo nchi jirani za Zambia na DR Congo ili kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo.
Ulega ametoa agizo hilo akiwa Tunduma mkoani Songwe na kueleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanayopitia wasafirishaji na wananchi wa eneo hilo kutokana na msongamano wa malori kwa muda mrefu na kukwamisha matumizi ya barabara kwa watumiaji wengine.
“Namuagiza Mkurugenzi kutoka TANROADS watafute fedha haraka ya dharura, pafanyike tathmini na tutapanua hapa mara moja ili zile njia tatu zijengwe hapa na kupunguza msongamano uliopo wa malori eneo hili”, amesema Ulega.
Kuhusu changamoto ya Mzani wa Mpemba unaosababisha magari kugeuza ili kupima uzito, Waziri Ulega amesema Wizara ya Ujenzi inakwenda kujenga mzani mwingine katika eneo la Iboya ili kuruhusu magari yote yanayotoka Tunduma kwenda Mbeya kupima uzito katika mzani huo na hivyo utapunguza msongamano wa malori.
“Kupitia mzani huo hakutakuwa na mambo ya kugeuza tena, Mzani wa Mpemba kazi yake itakuwa ni moja tu kupokea magari yanayotoka Mbeya kwenda Tunduma”, amesisitiza Ulega.
Aidha, Ulega amewataka Mameneja wa TANROAS wa mikoa ya Mbeya na Songwe kuhakikisha wanaimarisha barabara za mchepuo ambazo kwa kiasi kikubwa zitapunguza foleni ya magari katika ukanda huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya barabara katika mkoa huo na kumuomba Waziri wa Ujenzi kufanyia kazi mipango waliyoainisha ili kupunguza foleni eneo hilo.
Awali wakieleza changamoto za eneo hilo, madereva wa malori kwa nyakati tofauti wamesema miongoni mwa sababu zinazopelekea foleni kuwa kubwa ni mzani wa kupimia uzito wa malori kushindwa kuendana na wingi wa malori hivyo kumuomba Waziri Ulega kuona namna bora ya kuweka mizani ambayo itarahisisha upimaji wa uzito.







Post a Comment