SERIKALI YAONYA UDANGANYIFU WA MIRADI


Katibu tawala(DAS) Wilaya ya Chato, Thomas Dimme, akikabidhi mkopo wa pikipiki kwa kikundi cha bodaboda

............

CHATO

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imeonya udanganyifu wa baadhi ya miradi inayotekelezwa kupitia fedha za mikopo ya aslimia 10 za halmashauri ya wilaya hiyo, huku ikiwataka wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu kuwa na ubunifu wa miradi yenye tija.

Akikabidhi pikipiki saba aina ya Sanlg zilizotolewa kwa kikundi cha vijana wa bodaboda wa kata ya Makurugusi ikiwa ni mkopo usiona na riba, Katibu tawala wa wilaya hiyo, Thomas Dimme, ameonyesha kukerwa na baadhi ya wanufaika kuwa na miradi hewa na baadhi yao kukosa ubunifu wa miradi yenye tija.

Huku akitolewa mfano wa kikundi kilichodai kuwa na mradi wa ufugaji kuku lakini baada ya kufanya ziara ya kikazi kutembelea kikundi hicho hakufanikiwa kuona mifugo hao, huku viongozi wakimueleza kuwa kuku wamekufa siku chache kabla ya kiongozi huyo kufika eneo la mradi.

Kutokana na hali hiyo, amelazimika kutoa onyo kali kwa baadhi ya wanufaika kwa mikopo ya aslimia 10 inayotolewa kwa makundi ya Wanawake,Vijana na Wenye ulemavu kwa halmashauri zote nchini pamoja na maofisa wa serikali waliopewa jukumu la kuvisimamia vikundi hivyo.

Akizungumzia utolewaji wa pikipiki hizo zenye thamani ya Sh. 18,200,000 amesema mkopo huo uwe chachu ya kujikwamua kiuchumi kwa vijana hao ikiwa ni pamoja na kurejesha mikopo yao kwa uaminifu ili iwanufaishe na wengine zaidi.

Amesema nia ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa makundi lengwa ni njema sana na kwamba wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo za kujiondolea umaskini wa vipato.

Dimme, amesisitiza viongozi wa Idara ya maendeleo ya jamii kila kata kutumia muda na elimu zao kuwaelimisha wananchi namna bora ya kuibua miradi yenye tija katika jamii badala ya vikundi vingi kuwa na miradi inayofanana, hali inayoweza kupunguza ufanisi kiuchumi.

Ofisa maendeleo wa kata ya Makurugusi, Zawadi Enock, ameahidi kuvisimamia vyema vikundi vilivyopokea mikopo ya aslimia 10 kwenye Kata yake ili viweze kuwa mfano bora wa urejeshaji wa fedha za serikali kwa wakati na kuonyesha tija itakayopatikana kila mwaka.

Mmoja wa wanufaika wa mkopo huo ambaye pia ni Katibu wa kikundi hicho, Elias Jamonda, amempongeza Rais Samia kwa kutambua mahitaji ya vijana na kuamua kutenga fedha kupitia halmashauri za wilaya na Majiji nchini kwaajili ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aidha amedai kuwa kikundi hicho kinayo malengo makubwa ya kujiondolea umaskini kupitia mkopo huo na kwamba nimatarajio yao kumaliza kulipa mkopo huo ndani ya muda uliopangwa ili waweze kukopa zaidi.

Mikopo hiyo ni mwendelezo wa mingine ilivyotolewa kwa makundi mbalimbali ya Vijana, Wanawake na wenye Ulemavu ambao wanajishughulisha na kazi mbalimbali za kujipatia kipato halali wilayani humo.




 

0/Post a Comment/Comments