ULEGA AMSIMAMISHA KAZI ‘BOSI’TEMESA

::::::::

SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi imemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za uzembe, usimamizi dhaifu na ubadhirifu dhidi yake na viongozi wengine wa taasisi hiyo. 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza hatua hiyo jijini Dar es Salaam leo akisema hatua hiyo imefuatia malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji wa taasisi hiyo lakini pia matokeo ya uchunguzi wa tume iliyoundwa na vyombo vya serikali kuchunguza tuhuma hizo.

Ulega amesema wizara ilipokea barua kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo mbovu wa Temesa. Barua hiyo ilipitia kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kabla ya kufikishwa wizarani.

Ameeleza kuwa uchunguzi huo pia ulibaini ubadhirifu wa takribani Sh bilioni 2.5, na kuunda kamati maalumu iliyopewa siku saba kuchunguza. “Atakayebainika kuhusika, atafikishwa moja kwa moja mahakamani,” amesema Ulega.

Kufuatia uchunguzi huo wa vyombo, Ulega alisema sasa sheria itafuata mkondo wake kwa kuwahoji wahusika na kufanya uchunguzi wa ndani nak ama kutakuwa na tuhuma za makosa ya kijinai, wahusika watapelekwa katika vyombo vya sheria.

“Mara baada ya kupokea barua hiyo, tulifanya uchunguzi na kugundua kweli kulikuwa na uzembe. Ndipo tukachukua hatua za kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Temesa ambao hawakwenda sambamba na kasi ya maendeleo,” amesema.

Ameeleza kuwa uchunguzi huo pia ulibaini ubadhirifu wa takribani Sh bilioni 2.5, na kuunda kamati maalumu iliyopewa siku saba kuchunguza. “Atakayebainika kuhusika, atafikishwa moja kwa moja mahakamani,” amesema Ulega.

Ulega alikuwa katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa kivuko cha Nyinyi–Nyamisati kitakachotoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati, na kusema kuwa ujenzi huo uko nje ya muda waliokubaliana.

“Nimekuja kukagua mradi wa ujenzi wa meli ya abiria kutoka Nyamisati mpaka Mafia. Nimekuta mradi upo asilimia 57; bado mpo nyuma. Nawahimiza mchangamke. Nimesikia pia ujumbe wa Mbunge wa Kigamboni kuhusu msongamano kwenye vivuko kama pale Darajani, hivyo natoa maelekezo Katibu awasiliane na Katibu Mkuu wa Uchukuzi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema Ulega.

Ulega amesema taarifa aliyopewa inaonesha mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2025, lakini alipoiika kiwandani alielezwa kuwa utekelezaji wake utakamilika Mei 2026, huku hadi sasa ukiwa umefikia asilimia 57 tu.

Kivuko hicho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 300, tani 120 za mizigo pamoja na sehemu maalumu ya kuhifadhi maiti.

Ametoa kauli hiyo leo Desemba 7, 2025 katika eneo la Mji Mwema, Kigamboni, ambapo ujenzi wa kivuko hicho unaendelea. Amewataka mafundi na mkandarasi kuongeza kasi ya kazi kwa kuwa wakazi wa Mafia na Nyamisati wanakisubiri kwa hamu.

Amesema msongamano katika eneo la Darajani na Barabara ya Mandela unahitaji majadiliano ya kina ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa kuwa foleni hiyo imekuwa kero kwa wananchi.

Katika ziara hiyo pia ametembelea ujenzi wa daraja la Nguva lililopo Mtaa wa Kibaoni, Muongozo, na kuagiza ifikapo Januari liwe limekamilika.

Waziri Ulega amewataka mafundi kujirekodi wakati wakifanya kazi na kushiriki video hizo mtandaoni ili kuhamasisha vijana wengine kuona manufaa ya miradi ya serikali.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Temesa, Moses Rajabu, amesema mradi huo unagharimu Sh bilioni 9.4, na hadi sasa Sh bilioni 4.3 tayari zimetolewa.

Mbunge wa Kigamboni, Sanga Nyakisa, ameomba wizara kutatua changamoto za vivuko katika wilaya hiyo, akisema ni tatizo sugu linalowakabili wakazi hao.

“Najua serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma, lakini ombi letu sisi wa Kigamboni ni mambo mawili mbinafsishe vivuko au muharakishe malipo ya vivuko viwili MV Kigamboni na Kivukoni pamoja na matengenezo ya MV Kazi ambayo inafanya kazi saa 24,” amesema Sanga.






Mwisho
 

0/Post a Comment/Comments