WANAFUNZI 937,581 WAPANGIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA 2026


::::::::::

Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 937,581 watakaojiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2026, wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104. Hii ni hatua inayoonesha mafanikio makubwa katika kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu darasa la saba anaendelea na elimu ya sekondari.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, alisema wanafunzi wote wamepangwa katika shule za bweni na kutwa za serikali, kulingana na vigezo na mwongozo wa mwaka 2024.


Alibainisha kuwa shule za bweni zimegawanywa katika makundi matatu: shule za wanafunzi wenye ufaulu wa juu, shule za Amali, na shule za bweni za kitaifa, ambazo hupokea wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali kwa kuzingatia mgawanyo wa kitaifa.

Kwa shule za ufaulu wa juu, wanafunzi 815 wamechaguliwa, wakiwemo wasichana 335 na wavulana 480, na watasoma katika shule maarufu kama Ilboru, Msalato, Kibaha, Kilakala, Mzumbe, Tabora Boys na Tabora Girls, zinazojulikana kwa ushindani na nidhamu ya juu.

Aidha, shule za Amali zimepokea wanafunzi 3,441, huku shule za bweni za kitaifa zikichukua jumla ya wanafunzi 7,360, wakiwemo wasichana 5,014 na wavulana 2,346. Kwa shule za kutwa, wanafunzi 925,965 wamepangiwa kulingana na maeneo wanayotoka.

Profesa Shemdoe alisema maandalizi yote ya kuwaandaa wanafunzi kuanza muhula mpya yanaendelea vizuri, na wanafunzi wa bweni wanapaswa kuripoti Januari 12, 2026, huku wale wa kutwa wakitarajiwa Januari 13, 2026.

Alisisitiza umuhimu wa shule kutumia kipindi cha orientation kuwaimarisha wanafunzi katika mawasiliano na kuwasaidia kuchagua fani wanazopenda, sambamba na wazazi kuhakikisha watoto wao wanaandaliwa ipasavyo ili kuepuka kuchelewa.

Alihitimisha kwa kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, ambao umewezesha kila mwanafunzi kupata nafasi ya kuendelea na masomo bila changamoto za uhaba wa nafasi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.






0/Post a Comment/Comments