Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia mchakato wa upatikanaji wa ajira katika taasisi, idara na mashirika ya umma kwa uwazi, uwajibikaji na kuzingatia ushindani, kama inavyoelekezwa na sera ya ajira nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete, ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, serikali imetoa jumla ya vibali 41,500 vya ajira, ikiwa ni pamoja na nafasi mpya 12,000 zilizotengwa kwa ajili ya kuongeza nguvu kazi katika sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa Waziri Ridhiwani, kati ya nafasi hizo, 5,000 ni kwa kada ya afya, huku 7,000 zikiwa ni kwa ajili ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati, ili kuimarisha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi na kuinua kiwango cha elimu nchini.
Ameongeza kuwa usaili kwa ajili ya nafasi hizo unaanza kesho, Desemba 13, 2025, na kuwataka waombaji wote walioitwa kufuatilia taratibu na miongozo iliyotolewa ili kushiriki ipasavyo.
Katika hatua nyingine Kikwete amesema Ofisi hiyo imefanya marekebisho ya mifumo ikiwemo mfumo wa E-Mrejesho, ili kuwawezesha wananchi kutoa maoni na Kero kuhusu huduma za serikali na taasisi zake, ikiwa ni muendelezo wa kurahisisha huduma za kidigitali serikalini na kuwafikia wananchi wengi zaidi.





Post a Comment