Na Mwandishi Wetu, Handeni
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, ametoa wiki tatu kwa Halmashauri ya Mji Handeni kufanya maboresho mbalimbali katika Soko la Chogo, ikiwamo kurekebisha mageti ya kuingilia sokoni, ili kudhibiti tatizo la wizi wa bidhaa za wafanyabiashara.
Mhe. Nyamwese ametoa agizo hilo Januari 9, 2026, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko hilo na kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika mazingira safi, salama na rafiki, ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi bila hofu ya usalama wa mali zao.
Aidha, katika ziara hiyo, Mhe. Nyamwese ameelekeza Halmashauri ya Mji Handeni kufanya marekebisho ya haraka ya mageti ya kuingilia sokoni hapo ili kudhibiti wizi wa mara kwa mara wa bidhaa za wafanyabiashara, jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara kwao.
“Hali ya usafi katika lile dampo hairidhishi. Mrundikano wa taka uliopo unahatarisha afya za wananchi na wafanyabiashara. Naiagiza Halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wa soko kuangalia namna bora ya kuhakikisha taka zinaondolewa kwa haraka pindi zinapokusanywa,” ameagiza.
Naye, Afisa Biashara wa Halmashauri wa Mji Handeni, Paul Lusinde, ameahidi kufanyia kazi maagizo ya Mkuu huyo.
Post a Comment