.............
📌 USHIRIKI WA RAIS SAMIA KATIKA KUVITANGAZA VIVUTIO VYA UTALII NA UIMARISHAJI WA MINDOMBINU VYATAJWA.
Na Sixmund Begashe, Mikumi
Watalii wa ndani na nje wameendelea kuiamini na kuichagua Tanzania kama nchi salama ya kuitembelea kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali vya Utalii ambapo kwa mwaka 2025 pekee idadi ya Watalii imeongezeka kwa asilimia 9 ukilinganisha na mwaka Jana.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Mikumi Mkoani Morogoro, alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari, kwa lengo la kuelezea mafanikio ya serikali kupitia Wizara hiyo na mikakati ya kuendeleza uhifadhi na Utalii nchini.
Amesema kuwa sekta ya utalii ni moja ya sekta ya kimkakati na ya kimageuzi, kutokana na kuwa na mchango mkubwa unaoonekana na unaopimika katika uchumi wa Taifa.
"Mathalan, takwimu za sasa zinaonesha kuwa, Sekta ya utalii inachangia takribani asilimia 25 ya mauzo ya nje ya nchi na takriban asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP)". Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt Kijaji amesema kuwa, jamii haiwezi kuzungumzia mafanikio ya sekta ya utalii nchini pasipo kutambua jitihada za makusudi zilizofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuibeba sekta hiyo hususani filamu za kimkakati za Tanzania alizoshiriki: The Royal Tour na Amazing Tanzania ambazo zimeiweka nchi yetu kwenye ramani ya dunia.
"Jitihada zake zimechangia ongezeko la watalii wa kimataifa kwa asilimia 132.1, kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi 2,141,895 mwaka 2024. Aidha, watalii wa ndani wameongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi 3,218,352 mwaka 2024". Alisema Dkt. Kijaji
Ameongeza kuwa hatua hiyo imefanya jumla ya watalii waliotembelea vivutio mbalimbali nchini kufikia milioni 5.3 sawa na asilimia 116.02.
Aidha Dkt. Kijaji amefafanua kuwa, Wizara hiyo imeibua mazao mapya ya utalii ya kimkakati ambayo ni pamoja na Utalii wa mikutano na matukio (MICE Tourism), Utalii wa fukwe na bahari, Utalii wa kihistoria na urithi, Utalii wa michezo, Utalii wa utamaduni na Utalii wa Ikolojia ili kuchechemua utalii zaidi nchini.
Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Dkt. Kijaji, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema mkoa wa Morogoro umejipanga kuingia katika tatu bora ya mikoa inayopokea watalii wengi na kuingiza kiasi kikubwa cha mapato yatokanayo na mazao ya Utalii.
Mhe. Malima ameongeza kuwa kutokana na lengo hilo la Mkoa wa Morogoro, uongozi wa mkoa umetenga maeneo maalum kwa ajili ya kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza kwa lengo la kuendeleza Utalii.
Ameongeza kuwa kwa sasa mkoa huo unapokea watalii wengi wa ndani na nje ambao wanakosa maeneo ya kulala na hivyo kutoa wito kwa sekta binafsi, wadau wa Utalii na wananchi wenye uwezo kujitokeza na kuwekeza katika eneo la malazi hususani loji na Hoteli.






Post a Comment