Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mwaka 2026 imeendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kujenga na kufungua shule za awali na msingi za mchepuo wa Kiingereza ili kukidhi mahitaji ya wananchi waliokuwa wakihitaji huduma hiyo.
Miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu, ambayo tayari imekamilika na kuanza kutoa huduma. Shule hiyo imejengwa kwa gharama ya Shilingi 569,264,013.76 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri, ikiwa na miundombinu yote muhimu ikiwemo madarasa, madawati, vyoo na walimu wa kutosha.
Aidha, Shule ya Msingi Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe bado iko katika hatua za ukamilishaji wa ujenzi. Hadi sasa jumla ya Shilingi 252,897,072.40 tayari zimepelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, huku Shilingi 151,760,000.00 zikitarajiwa kupelekwa ili kukamilisha ujenzi.
Wananchi wa Manispaa ya Kibaha wamempongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa juhudi na mipango madhubuti inayolenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora, hususan elimu ya mchepuo wa Kiingereza, bila kuwalazimu wazazi kugharamia ada kubwa katika shule binafsi.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Dkt. Shemwelekwa amesema kuwa uanzishwaji wa shule hizo ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri wa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora katika mazingira rafiki na salama. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi hadi kukamilika kwa Shule ya Msingi Mwambisi ili ianze kutoa huduma kama ilivyopangwa.




Post a Comment