NAIBU WAZIRI MAJI ACHARUKA MKANDARASI KUTELEKEZA MRADI CHATO

............

CHATO

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameagiza kukatwa fedha za mkandarasi wa kampuni ya "Peritus Exim Infrastructure Co. LTD" iliyokuwa ikitekeleza ujenzi wa mradi wa maji taka wilayani Chato mkoani Geita kutokana na kukiuka mkataba.

Kwa mujibu wa mkataba huo mkandarasi alipaswa kuanza ujenzi juni 23, 2023 na kukamilisha Desemba 20, 2024.

Lakini Kutokana na sababu zisizo fahamika mkandarasi huyo ametelekeza mradi huo huku akiwa amelipwa kiasi cha fedha za serikali na kutokomea kusikojulikana.

Kutokana na hali hiyo, Mhandisi Mathew amelazimika kutembelea eneo hilo na kujionea kwa macho yake kisha kutoa kauli ya serikali kwa mkandarasi huyo.

Akizungumza na wananchi wa Buzirayombo baada ya kumaliza kutembelea mradi mkubwa wa maji wa miji 28 nchini unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 168,000 wilayani Chato, Mhandisi Mathew, amesema serikali haiwezi kuendelea kufumbia macho uzembe wa namna hiyo unaodhoofisha jitihada kubwa za serikali ya awamu ya sita.

" Kwanza nilipofika tu kwenye chanzo cha mradi wenyewe nimekuta kreki nyingi sana kabla hata mradi wenyewe bado haujaanza kutumika, mradi umejengwa chini ya kiwango,lakini pia mkandarasi hayupo hata eneo la mradi wakati alishalipwa kiasi cha zaidi ya milioni 800 kati ya Shilingi Bilioni 1.5 zilizokuwa kwenye mkataba".

"Kampuni hii imekuwa ikituchezea sana kwenye miradi yetu, imeharibu pia Tabora na Igunga kote anafanya mchezo huu, sasa haiwezekani tena kufanya kazi za namna hii, nimemuagiza Katibu wizara ya maji kufanya utaratibu wa kuanza kumkata fedha ili alipe fidia ya kuchelewesha kazi",

"Na nimemwagiza Katibu atazame namna ya kumfuta mkandarasi huyo kutekeleza ujenzi wa miradi ya wizara ya maji nchini, na mradi huu ulipaswa kuwa na gari mbili lakini hakuna hata moja" amesema Mhandisi Mathew.

Hata hivyo, Waziri Mathew ameupongeza mradi mkubwa wa maji wa miji 28 nchini kutokana na ubora na usimamizi mzuri ambao inaonyesha wazi thamani ya pesa za serikali.

Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 40 unatarajiwa kuwa mwarobaini wa changamoto ya hupatikani wa maji safi na salama kwa wananchi na kwamba unatarajiwa kukamilika ifikapo September 30, 2026.

Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Chato (Chawassa) Mhandisi Isack Mgeni, amesema mbali na mji wa Chato mradi huo kutokana na ukiwa wake pia utaweza kuwahudumia wananchi wengine wa miji ya Muganza na Bwanga.

Aidha amesema kwa sasa wananchi wa mji wa Chato wanapata huduma ya maji safi kwa aslimia 71 na kwamba kukamilika kwa mradi huo zaidi ya aslimia 100 watapata maji safi na salama pasipo usumbufu wa namna yoyote.

                         Mwisho.




 

0/Post a Comment/Comments