:::::::
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema hali mbaya ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza ilisababisha kuchelewa kwa safari ya ndege namba TC102 kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, baada ya rubani kushindwa kutua mara mbili kwa sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumapili na ATCL, ndege aina ya Boeing 737-9 MAX iliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa muda uliopangwa ikiwa na abiria 165.
Hata hivyo, ilipokaribia Mwanza, hali ya hewa ilibainika kuwa si salama kwa kutua. Kwa kuzingatia taratibu za usalama wa anga, rubani alifanya majaribio mawili ya kutua bila mafanikio kabla ya kuwasiliana na mamlaka za uongozaji ndege na kuamua kuielekeza ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kusubiri hali ya hewa kuimarika.
Ndege hiyo ilitua salama KIA na kukaa kwa takribani saa tatu na nusu. ATCL ilisema uamuzi huo ulifanywa kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa vya usalama wa safari za anga, huku usalama wa abiria ukipewa kipaumbele cha juu.
Baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuthibitisha kuimarika kwa hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ndege iliondoka KIA kuelekea Mwanza na kutua salama majira ya saa 11:24 alfajiri.
Hakuna majeruhi wala hitilafu ya kiufundi iliyoripotiwa.
ATCL ilieleza kuwa ilitoa huduma kwa abiria wote waliokuwa ndani ya ndege wakati wa kusubiri, kwa mujibu wa taratibu za kampuni. Shirika hilo pia limeomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na kuchelewa kwa safari hiyo na kusisitiza kuwa maamuzi yote yalifanywa kwa maslahi ya usalama wa abiria na wafanyakazi wa ndege.

Post a Comment