"Afya ni taji hakuna aijuae isipokuwa mwenye maradhi" huo ni msemo wa wahenga wakisisitiza umuhimu wa jamii kuthamini utimamu wa mwili pasipo kutazama ukubwa wa gharama.
Ukweli huo unaungwa mkono na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya awamu ya kwanza kutenga zaidi ya bilioni 28 kwaajili ya kuhudumia watu wasiojiweza takribani 1,457,602 ambao ni sawa na kaya 276,004, ambapo wazee ni 229 na watoto 267 nchini.
Wanufaika hao wataingizwa katika mkakati wa mfumo wa bima ya afya kwa wote, hali itakayosaidia kuondoa changamoto ya matibabu kwa makundi hayo muhimu.
Katika mkakati wa serikali ya awamu ya sita kuboresha huduma za afya nchini, wilaya ya Chato mkoani Geita haikubaki nyuma baada ya kuzindua mpango kazi kwaajili ya kuanza usajili wa walengwa ikiwemo kundi la wazee, watoto, wajawazito na watu wenye Ulemavu.
Mkakati huo umezinduliwa rasmi leo na mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Peter Bura, baada ya kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo, wakuu wa Idara na vitengo wa halmashauri hiyo, watendaji wa kata, walimu wakuu wa shule za msingi pamoja na Sekondari.
Wengine ni maofisa maendeleo ya jamii kata, maofisa ustawi wa jamii kata na baadhi ya wadau wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Bura amesema serikali ya awamu ya sita ina dhamira ya dhati kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha inaboresha afya zao ili kuwa na jamii yenye afya, nguvu na amani.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chato, Mandia Kihiyo, ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia kwa kuwezesha ujenzi wa vituo vya kutolea huduma 17 ndani ya kipindi cha miaka minne ya utawala wake.
Amesema ongezeko hilo litasaidia upatikanaji wa matibabu ya uhakika na kwa haraka zaidi, hivyo wananchi hawana budi kujiunga na bima ya afya kwa wote.
Aidha amesema kwa sasa upatikanaji wa huduma za dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya umefikia aslimia 90 jambo linalopaswa kupongezwa.
Baadhi ya wadau katika kikao hicho wameiomba serikali kuwahisha miongozo ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ili kupunguza hofu zilizojengeka katika jamii ikiwemo upatikanaji huduma hiyo kwa wanafunzi.



Post a Comment