📌Bima ya afya kwa wote yaguswa
Na Augusta Njoji
KAMATI ya Ushauri ya Wilaya ya Handeni (DCC) imepitisha mapendekezo ya rasimu ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Sh. bilioni 35 kwa mwaka wa fedha 2026/27 ya Halmashauri ya Mji Handeni, huku miongoni wa vipaumbele vilivyotajwa ni pamoja na kugharamia Bima ya Afya kwa Wote kwa wananchi wasio na uwezo kwa kutumia mapato ya ndani.
Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika leo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amewaagiza Watendaji wa Kata, Mitaa pamoja na Wahudumu wa Afya kutoa elimu kwa wananchi kwa lugha rahisi ili wahamasike kujiunga na mpango huo wa bima ya afya.
Amesema serikali tayari imetangaza kuanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, hivyo ni wajibu wa viongozi na watendaji kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wake ili wawe na uhakika wa matibabu wanapohitaji huduma za afya.
“Ni lazima wananchi waelimishwe kwa lugha wanayoielewa ili wajue faida za bima hii, kwani itawasaidia kupata huduma za matibabu kwa uhakika,” amesema Mhe. Nyamwese.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kubaini kama inatekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha, sambamba na kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema rasimu ya mpango na bajeti imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi na mikakati ya maendeleo ya Halmashauri.
Ametaja vipaumbele vingine vitakavyotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani kuwa ni pamoja na kutenga Sh milioni 176 kwa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ujenzi wa fremu za maduka ili kuongeza vyanzo vya mapato, utekelezaji wa afua za lishe, ujenzi wa maabara katika shule moja ya sekondari pamoja na kuboresha miundombinu ya mifugo.
Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Hudi Muradi, amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 Sh milioni 30 zimetengwa katika mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa wananchi wasio na uwezo na kwamba kwasasa serikali inaendelea na zoezi la uhakiki wa wananchi hao.
Ameongeza kuwa serikali imeimarisha miundombinu ya afya na kuajiri watumishi wapya 58 ili kuboresha utoaji wa huduma katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Post a Comment