Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wamiliki na waendeshaji wote wa Bandari Kavu nchini (ICD) kuanza kufanya kazi kwa saa 24 ili kuendana na kasi ya utoaji huduma za Forodha na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Akizungumza leo Februari 19, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao cha pamoja na wamiliki wa ICD, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema utekelezaji wa utaratibu huo utarahisisha biashara, kuondoa msongamano wa mizigo na kuongeza tija katika sekta ya usafirishaji na ugavi.
Mwenda amesema TRA ipo tayari kuwezesha kuanza kwa utaratibu huo, akibainisha kuwa kwa upande wa watumishi wa Forodha, huduma za saa 24 tayari zimeanza kutolewa.
“Niwatake kuhakikisha mnaongeza ufanisi katika ufanyaji wenu wa kazi kwa kujipanga kutoa huduma kwa saa 24. Sisi kama TRA tutatoa wafanyakazi wetu, nanyi kwa upande wenu mjipange kwa vifaa na mahitaji mengineyo; lengo ni kuongeza ufanisi,” amesema Mwenda.
Amesema anatambua umuhimu wa ICD na mchango wake katika makusanyo ya kodi, akieleza kuwa bandari hizo zimekuwa kiungo muhimu katika kurahisisha biashara ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesisitiza kuwa ufanisi wa Bandari Kavu unakwenda sambamba na ufanisi wa Forodha, hivyo ni wajibu wa wamiliki kushirikiana na TRA kuhakikisha malengo ya pamoja yanafikiwa. Amewapongeza waendeshaji hao kwa kazi wanayoifanya katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
AONYA UKWEPAJI KODI
Katika hatua nyingine, Kamishna Mkuu Mwenda ameonya vitendo vya ukwepaji kodi vinavyofanywa na baadhi ya wamiliki wa ICD, akisisitiza kuwa TRA inazo taarifa za vitendo hivyo na haitasita kuchukua hatua kali za kisheria.
“Natambua kuna ukwepaji kodi katika ICD. Hii haiwezi kukubalika. ICD zote zinatakiwa kuzingatia sheria. Ni lazima tushirikiane kuzifanya ICD zionekane kuwa salama; hatutosita kuchukua hatua kwa wale watakaobainika,” amesisitiza Mwenda.
SEKTA BINAFSI YASISITIZA USHIRIKIANO
Kwa upande wake, Rais wa Sekta Binafsi (TPSF), Bi. Angelina Ngalula, amesema waendeshaji wa Bandari Kavu ni kiungo muhimu katika safari ya kuelekea Dira ya Taifa ya 2050, hivyo wanapaswa kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kujenga uchumi imara na kuleta mageuzi chanya.
Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Bandari Kavu, Bw. Meleckzedeki Kichange, amepongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali kwa upande wa Forodha, ikiwemo TANCIS, akisema imerahisisha utengaji wa kazi na kuongeza ufanisi.
Amesema wamiliki wa ICD wameendelea kushirikiana kwa karibu na TRA kama mdau wao mkuu, na kwamba kwa sasa wanafanya kazi katika mazingira ya amani na utulivu zaidi kuliko kipindi chochote kilichopita.
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Bw. Juma Bakari, amesema asilimia 52 ya mapato ya forodha yanatokana na Bandari Kavu, akisisitiza kuwa wako tayari kuwezesha mazingira bora ya utendaji kazi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika mapato ya Serikali.
= = = = = =

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Post a Comment