LUTANDULA AIHESHIMISHA BUKIRIGURU UJENZI WA ZAHANATI ILIYOKWAMA MIAKA 24


Mbunge Pascal Lutandula, akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chato Kusini.
Mbunge akiwakabidhi wananchi mabati ya ujenzi wa Zahanati ya Bukiriguru
Jengo la Zahanati ya Kijiji lililokwama kwa miaka 24
...........

CHATO

"Unaweza kusema mfupa mgumu uliomshinda fisi sasa umetafunika" ni ndani ya siku 100 za Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini, Pascal Lukas Lutandula, kufanikiwa kutatua kero ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Bukiriguru iliyodumu kwa miaka 24 pasipo kukamilika.

Ni baada ya wananchi kuanzisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji chao tangu mwaka 2002 na kushindwa kukamilika muda wote licha ya ahadi ya serikali kukamilisha maboma yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Hatua hiyo imekuwa mwiba mchungu kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakipokea kero hiyo na kushindwa kuitekeleza licha ya mateso makubwa ya wananchi hasa wajawazito na watoto wachanga.

Kutokana na hali hiyo, katika kampeni za Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2025, aliyekuwa mgombea wa Ubunge kwenye Jimbo la Chato Kusini, Lutandula akawaahidi wananchi wa Kijiji hicho kuwa iwapo atapata ridhaa ya kuwaongoza atakamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo ndani ya siku 100 za Ubunge wake.

Hata hivyo, zikiwa zimesalia siku sita kutimia siku 100 za uongozi wake, amelazimika kuwakabidhi wananchi wa Kijiji hicho mabati 205 kupitia fedha zake binafsi ili kuhakikisha anatatua kero hiyo kama alivyowaahidi wakati wa mchakato wa kampeni za Uchaguzi mkuu.

Hayo yamefanyika wakati Mbunge huyo akiwa kwenye mkutano wa mapokezi ya mitambo ya kuchonga barabara za wananchi wa Jimbo lake uliofanyika mjini Bwanga, na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi ambao mbali na mambo mengine wameshuhudia utolewaji wa mabati hayo kwa jamii.

"Jamani haya yote ninafanya kwa fedha zangu mwenyewe, nilikuwa naweza kuzipeleka popote hata kama ni kuoa mhindi wala msingeniuliza chochote, nafanya hivi kwa sababu ya upendo wangu kwenu" amesema Lutandula.

Diwani wa kata ya Bwanga, Sanane Chai, amempongeza Mbunge huyo kwa kutimiza ahadi rukuki alizoahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi mkuu wa 2025 huku akiwasisitiza wananchi kuendelea kumwombea mema ili mengi mazuri ayalete kwa wananchi wake.

Amesema kwa muda mfupi wa siku 100 za Ubunge wake, amesaidia kuezeka vyumba vya madarasa, Zahanati pamoja na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa jimbo hilo.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bwera, Josephat Manyenye, ameuhakikishia umati uliojitokeza hapo kuwa hawakukosea kumchangua Lutandula kwa kuwa anasema na kutenda.

Amewasihi kumuunga mkono Mbunge wao iwapo wanahitaji maendeleo ya kweli na kwamba ni viongozi wachache sana wanaozaliwa na uchungu wa changamoto za wananchi kiasi cha kutumia fedha binafsi kwa manufaa ya jamii.

                          Mwisho.
 

0/Post a Comment/Comments