Na Carlos Claudio, Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Jesca Mbogo, ametoa wito kwa wanawake wa Wilaya ya Kondoa kuhamasisha usajili wa wasichana katika Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ili kuhakikisha kizazi kipya cha viongozi kinaandaliwa mapema.
Akizungumza katika ziara yake ya kwanza wilayani humo mara baada ya kuchaguliwa, Mhe. Mbogo alisema ipo haja ya kuingiza wasichana wengi zaidi ndani ya jumuiya hiyo ili kuimarisha uhai na mustakabali wa UWT.
“Tumeendelea kubaki sisi wenyewe na umri unaenda.
Nikirudi tena hapa, nataka nikute mmeingiza wasichana wengi zaidi. Nitaleta simu kwa ajili ya kuwasajili na tutashindana kata kwa kata kuona nani ataongoza kwa kuingiza wanachama wapya,” alisema Mbogo.
Alisisitiza kuwa malezi ya viongozi huanzia mapema, akieleza kuwa naye alilelewa na wanawake waliomtangulia hadi kufikia nafasi ya uongozi aliyonayo sasa.
“Nilivyokuwa mdogo nililea na kuongozwa na wanawake waliotutangulia hadi nikawa kiongozi bora. Sasa ni jukumu letu kuwalea wasichana wetu ili wawe viongozi bora wa kesho. Hii jumuiya tutamuachia nani kama hatutawaandaa?” alihoji.
Katika kuunga mkono juhudi za maendeleo, Mhe. Mbogo alichangia mifuko 10 ya saruji pamoja na shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa jumuiya hiyo wilayani humo.
Mbali na masuala ya ujenzi na uhai wa jumuiya, Mbunge huyo alitoa wito wa maridhiano miongoni mwa wanawake kufuatia kumalizika kwa uchaguzi.
“Naomba tusameheane. Hakuna aliyekuwa mkamilifu wakati wa uchaguzi. Kulikuwa na kusemana na kubishana, lakini sasa uchaguzi umekwisha, tubaki wanawake wa Kondoa na tuanze upya,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa ushirikiano ni msingi wa maendeleo, akibainisha kuwa pasipo kusameheana, kazi haiwezi kufanyika kwa ufanisi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mbogo alitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kumsogeza mwanamke mbele kielimu.
Alikabidhi mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi na kushiriki zoezi la upandaji miti kuunga mkono kampeni ya “Dodoma ya Kijani” iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia.
Aidha, Mbunge huyo alitangaza kuanzisha taasisi iitwayo Legal Women and Children Support yenye lengo la kusaidia wanawake na watoto katika masuala ya kisheria na haki zao.
Akihitimisha hotuba yake, aliwaomba wananchi wa Kondoa kumpa ushirikiano katika kutekeleza malengo yake ya maendeleo.




Post a Comment