Na Saidi Lufune, Dodoma
Idara ya Misitu na Nyuki imetakiwa kuweka mikakati ya makusudi ya kuongeza kiwango cha uzalishaji na uuzaji wa asali nje ya nchi ili kuongeza manufaa ya kiuchumi na ukuzaji wa Pato la Taifa.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) katika kikao kazi na Wataalam wa Sekta ya Nyuki na kuongeza kuwa sekta hiyo ni mojawapo ya sekta tegemezi katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, hivyo ni vyema kuongeza jitihada ya uzalishaji wa mazao ya nyuki hasa asali ili kuongeza uzalishaji kutoka 24% inayozalishwa sasa hadi kufikia 50% mwaka 2027.
Aidha, ameilekeza Idara hiyo kuendelea kufanya tafiti mbalimbali juu ya miti aina ya Mtonga bahari na Mikarafuu kubaini uwezo wa mimea hiyo kuzalisha asali yenye upekee kwa manufaa ya jamii ya wafugaji na Taifa kwa ujumla
Vilevile, Mhe. Chande ameisisitiza Idara hiyo, kushirikiana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Vyuo vya mafunzo na wadau wa Ufugaji Nyuki kufanya tafiti za kina juu ya utoaji wa huduma ya tiba nyuki kwa lengo la kuendelea kukuza wigo wa huduma zitokanazo na nyuki kwa jamii
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Bw. Seleboni Mushi amesema Wizara kupitia Idara hiyo inaendelea kushirikiana na Vyuo, Taasisi zilizo chini ya Wizara na wadau kuelimisha jamii kuhusu mbinu bora ya Ufugaji Nyuki kupitia utekelezaji wa “Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania iliyo Bora”, warsha na maonesho mbalimbali.





Post a Comment