Aibuka na kura 257, Dunga aibua mashaka
Mirambo Yusuf amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kupata kura 257 katika uchaguzi uliofanyika usiku wa kuamkia leo Jumapili, Februari 22, 2026.
Uchaguzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Lekham, Buguruni, jijini Dar es Salaam, wakati wa Mkutano Mkuu wa dharura wa Chama cha Wananchi (CUF) uliowakutanisha wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Katika matokeo hayo, Mirambo alimshinda mshindani wake wa karibu, Othman Omar Dunga, aliyepata kura 177. Hata hivyo, Dunga alionesha wasiwasi wake kuhusu baadhi ya wajumbe walioshiriki katika upigaji kura huo, akidai kuwa kwa mtazamo wake wengi wao hawakuwa wajumbe halali.
Mirambo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kigoma Mjini, anakuwa Mwenyekiti wa nne wa chama hicho, akirithi mikoba ya aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Katika kinyang’anyiro hicho, mgombea wa tatu, Nkunyunyika Siwale, alipata kura sita kati ya kura 448 zilizopigwa, huku kura sita zikiharibika.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Miraji Mtibwiliko aliibuka mshindi kwa kupata kura 264, akiwashinda Mohammed Ngulangwa aliyepata kura 88 na Mussa Mbarouk aliyepata kura 82.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Haroub Mohamed Shamsi alichaguliwa baada ya kupata kura 256, akimshinda Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 171. Mgombea mwingine, Amina Rashid Salim, alijitoa kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.
Uchaguzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika mustakabali wa uongozi wa CUF, huku macho yakielekezwa kwa mwenyekiti mpya katika kuimarisha umoja na mwelekeo wa chama hicho kuelekea chaguzi zijazo.
Credit by Mwananchi digital

Post a Comment