Makamu wa Rais wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amezitaka sekta binafsi nchini kushirikiana kwa karibu na vyuo vya elimu ya juu na vya ufundi, pamoja na kuwekeza katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia, ili kuinua viwango vya tafiti na kuboresha ubora wa elimu nchini.
Dkt. Nchimbi alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Alisema kupitia mpango huo, sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti mbalimbali pamoja na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani zinazohitajika sokoni, kulingana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Aidha, Makamu wa Rais alizitaka Taasisi za elimu na sekta binafsi kuzingatia kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa mpango huo, akisisitiza umuhimu wa kubaini mapema ujuzi unaohitajika sasa na siku zijazo.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo unapaswa kuzingatia zaidi fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu, ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kushindana na kupata fursa za ajira katika soko la ndani na kimataifa.
Dkt. Nchimbi alisema ushirikiano kati ya Taasisi za elimu na viwanda ni jambo la lazima katika dunia ya sasa, akieleza kuwa vyuo haviwezi kuendelea kuwa visiwa vya nadharia pekee, huku viwanda navyo vikishindwa kukua bila nguvukazi yenye ujuzi unaoendana na teknolojia na ushindani wa soko.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa vijana na wahitimu wa ngazi mbalimbali, ikitambua kuwa maendeleo endelevu ya Taifa hayawezekani bila rasilimaliwatu iliyoelimika na yenye tija.
Makamu wa Rais alisema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera na mitaala ya elimu katika ngazi zote, kwa lengo la kujenga mfumo wa elimu ulio mnyumbufu, jumuishi na unaoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira, sambamba na mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Uzinduzi wa mpango huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo aliahidi kuanzisha mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu, ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.
Kwa mujibu wa Dkt. Nchimbi, mpango huo unalenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya utoaji wa elimu na utendaji kazi, kwa kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele za Taifa zikiwemo nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na viwanda vya kuongeza thamani.
Alisema mpango huo unaweka msingi wa kujenga kizazi cha wahitimu wenye uwezo wa kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa, kwa kubadilisha mfumo wa elimu ya nadharia kwenda elimu inayozingatia ujuzi, vitendo, ubunifu na uzalishaji mali.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Dini, pamoja na wadau wa maendeleo, waajiri, wamiliki wa viwanda, wakuu wa taasisi na vyuo, pamoja na wanafunzi.
Makamu wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam kwaajili ya Uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (kulia) pamoja na Viongozi mbalimbali, wakionesha Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda mara baada ya kuuzindua katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, akiwa na Viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na baadhi ya Waajiri, mara baada ya kuzindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.



.jpg)
.jpg)

Post a Comment