NEMC YAPOKEA MAABARA TEMBEZI YA SH. MILIONI 715

::::::::

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limepokea gari maalum lenye maabara inayotembea kutoka Ubalozi wa Sweden kwa lengo la kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Februari 19, 2026 jijini Dar es Salaam, yakihudhuriwa na viongozi wa NEMC na wawakilishi wa Sweden.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Immaculate Semesi, amesema kabla ya msaada huo baraza lilikuwa likitumia muda na gharama kubwa kupeleka sampuli katika maabara zilizothibitishwa.

Amesema maabara hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 715 itapunguza gharama, kuokoa muda na kuongeza ubora wa maamuzi ya kitaalamu kwa kuwa upimaji utafanyika papo hapo eneo la tukio.

Dkt. Semesi amefafanua kuwa maabara hiyo inaweza kupima hali ya hewa, viwango vya sauti, mitetemo, afya ya maji pamoja na ubora wa udongo kwa wakati mmoja.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi, Paul Kalokola, amesema gari hilo lina vifaa vya kisasa ikiwemo droni zitakazosaidia kufikia maeneo magumu na yaliyofichika.

Naye Meneja wa Programu za Mazingira na Hali ya Hewa kutoka Ubalozi wa Sweden, Stephen Mwakifwamba, amesema mradi huo wa miaka mitatu ulikuwa na thamani ya dola milioni tatu za Marekani na umehusisha pia uboreshaji na tafsiri ya sheria za mazingira kwa Kiswahili.

Ameitaka NEMC kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, huku Serikali ya Sweden ikihaidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu.





0/Post a Comment/Comments