POLISI MBEYA WAWAKAMATA WAWILI KESI YA MAUAJI ITUMBI

::::::::::

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa taarifa kuhusu tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Itumbi, Elia Richard Sambala (53), mkazi wa Itumbi wilayani Chunya, yaliyotokea Februari 11, 2026.

Kwa mujibu wa polisi, saa 7 mchana Sambala alikutwa shambani kwake akiwa amejeruhiwa vibaya kichwani kwa kukatwa na kitu chenye makali na watu wasiojulikana. Alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya amesema mara baada ya tukio hilo, askari wa upelelezi walianza msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili kuhusiana na tukio hilo, huku juhudi za kuwabaini na kuwakamata wengine zikiendelea.

Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa masilahi katika eneo la uchimbaji madini ya dhahabu, ambapo mmoja wa wanafamilia alidaiwa kukodisha eneo kwa wawekezaji raia wa China bila kuwashirikisha ndugu wengine.

Aidha, polisi wametoa onyo kwa mtu anayejinasibu kuhusika na tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii na kujitambulisha kama kiongozi wa kikundi kiitwacho TFF (Tanzania Freedom Fighters), wakimtaka kuacha kupotosha umma huku juhudi za kumkamata zikiendelea.


 

0/Post a Comment/Comments