::::::::::
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha Sheria ya Elimu ili iendane na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023 pamoja na maboresho ya mitaala.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Februari 13, 2026, alimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, **Adolf Mkenda**, katika kikao cha wadau wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) kilicholenga kutoa maoni kuhusu mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353.
Alisema utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 unagusa ngazi zote za elimu na mafunzo nchini. Hivyo, Wizara inaendelea na tathmini ya Sheria ya Elimu pamoja na sheria za taasisi zilizo chini yake ili kuongeza tija na ufanisi.
Alibainisha kuwa pamoja na uwepo wa sera, utekelezaji wake unahitaji nyenzo muhimu ikiwemo sheria iliyoboreshwa. Aliwashukuru wadau kwa kuendelea kutoa maoni yatakayosaidia kuimarisha sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Martha Makala, alisema mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, Sura ya 353, ni fursa ya kujenga Tanzania yenye elimu jumuishi, haki na ubora.
Alisema marekebisho hayo yatasaidia kulinda watoto na wanafunzi pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira. Pia aliipongeza Wizara kwa kuwashirikisha wadau katika mchakato huo.
Martha alitaja maeneo yanayohitaji maboresho kuwa ni pamoja na suala la wanafunzi kukatisha masomo. Alipendekeza kuwepo kwa kifungu cha sheria kitakachohakikisha wanafunzi waliokatisha masomo wanarejeshwa na kumaliza mzunguko wao wa elimu.
Aidha, alipendekeza elimu ya lazima ya miaka 10 iwekwe kisheria ili iwe endelevu. Pia elimu bila ada na suala la lishe shuleni viwekwe kisheria ili kuongeza uwajibikaji kwa wazazi na walezi.
Alisisitiza kufanyika kwa marekebisho ili kuondoa ukinzani kati ya Sheria ya Ndoa na sheria za elimu, pamoja na kuhakikisha uendelevu wa Bodi ya Kitaaluma ya Walimu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, Profesa Saudin Mwakaje, alisema lengo la mapitio hayo ni kuimarisha mifumo ya kijamii na kiuchumi na kukidhi mahitaji ya mabadiliko mapya.
Aliongeza kuwa marekebisho hayo yatazingatia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na uhalisia wa soko la ajira.
Wakichangia maoni yao, baadhi ya wadau waliomba Wizara iangalie upya suala la masomo ya ziada (tuition). Walisema baadhi ya walimu hutumia vipindi hivyo kufundisha mada zinazopaswa kufundishwa darasani, jambo linalowaathiri wanafunzi wasioweza kumudu gharama.
Vilevile, wadau walipendekeza lugha ya alama ifundishwe kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kurahisisha mawasiliano katika huduma za jamii kama hospitali na masoko.











Post a Comment