SERIKALI KUNUSURU NGUVU ZA WANANCHI MABOMA YA ZAHANATI CHATO

..............

CHATO

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imeahidi kutenga fedha ili kuyahudumia maboma ya Zahanati yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kwa lengo kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Diwani wa kata ya Minkoto, Paulo Mfanis, kuiomba halmashauri ya wilaya hiyo kusaidia ukamilishaji wa jengo pekee la zahanati ya Kijiji cha Minkoto ambalo limepauliwa na kushindwa kuezekwa paa.

Hatua hiyo ambayo imeombwa kutazamwa kwa udharura wake inalenga kunusuru nguvu za wananchi walizochagia katika ujenzi huo na kwamba pasipo kuchukuliwa hatua za haraka huenda mbao zilizotumika kupaua majengo hayo zikaharibika bure.

Aidha Diwani huyo amesema kata yake haina kituo chochote cha afya wala zahanati, jambo linaloweka rehani maisha ya wananchi, na kwamba ipo haja kubwa kwa serikali kuitazama kata hiyo kwa jicho la huruma.

Ametoa hoja hiyo kwenye kikao cha robo ya pili cha Baraza la madiwani kilichoketi leo February 4,2026 kwa lengo la kujadili hoja mbalimbali zenye maslahi mapana kwa umma. 

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mandia Kihiyo, amelazimika kuahidi kufika eneo hilo na kutazama hali ilivyo ili kuweka nguvu kubwa katika kunusuru hali iliyopo.

Mbali na hilo, amesema halmashauri itaendelea kuhudumia maboma yote ya Zahanati yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ili kuhakikisha wanaungana na jitihada za jamii kujiletea maendeleo na kuondoa adha zilizopo katika maeneo yao.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Christian Manunga, amemuagiza mganga mkuu wa wilaya(DMO) pamoja na Mhandisi wa halmashauri hiyo, kufika haraka katika kata ya Minkoto ili kutafuta ufumbuzi wa haraka katika kunusuru nguvu za wananchi.

"Katika hili naomba kutoa maagizo, kwa udharura huu kuanzia kesho mganga mkuu na Mhandisi wa wilaya fikeni haraka Minkoto ili mkatazame namna bora ya kuweza kuleta ushauri wenye manufaa kwa mkurugenzi ili tunusuru nguvu za wananchi" amesema Manunga.

Ikumbukwe kuwa siku chache zilizopita halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita imepitisha makadilio ya bajeti ya Shilingi Bilioni 67 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umma.

                      Mwisho.

 

0/Post a Comment/Comments