SERIKALI YAITAKA CHAWASSA KUKUSANYA MAPATO ZAIDI


............

CHATO

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imeipongeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa mazingira mjini Chato (Chawassa) kwa kufanikiwa kuboresha maslahi ya watumishi wake, kutatua changamoto za upatikanaji wa maji kwa wateja pamoja na kununua pikipiki tano kati ya 10 zinazotarajiwa.

Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura, aliyewakilishwa na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Thomas Dimme, kwenye hafra fupi ya kugawa pikipiki tano mpya zilizonunuliwa na mamlaka hiyo ili kuboresha utendaji kazi, amesema Ofisi yake inaridhishwa na usimamizi mzuri uliosaidia kupunguza changamoto za malalamiko ya wateja ukilinganisha na awali

Aidha amewataka watumishi hao kutanguliza mbele uzalendo na utu wa kuwatumikia wananchi huku akisisitiza suala la ukusanyaji mapato ya mamlaka hiyo ili iweze kujiendesha kwa faida.

Kadhalika amemtaka mkurugenzi wa mamlaka hiyo kuwatambua watumishi wake wanaofanya kazi vizuri na kuwapatia zawadi ya fedha au vyeti vya utambuzi wa kazi zao hali itakayoongeza ufanisi kazini.

Kwa upande Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Isack Mgeni, mbali na kuipongeza serikali kwa kuipatia mamlaka hiyo fedha za uendeshaji wa taasisi hiyo, amesema kumefanyika maboresho makubwa ya kiutendaji ikiwemo maslahi ya watumishi kutoka Tsh. 50,000 za awali hadi kufikia Tsh. 200,000 kwa mwezi.

Aidha amedai upatikanaji wa pikipiki hizo utasaidia kuwafikia wateja kwa haraka lengo likiwa ni kutatua changamoto za maji na ukusanyaji mapato ya taasisi badala ya kuendelea kutumia baiskeli ambazo zimekuwa zikisababisha kuchelewa na na kupunguza utimamu wa kazi.

Mgeni amesema wakati anakabidhiwa taasisi hiyo, alikuta ukusanyaji mapato ukiwa chini ya Tsh. 40 milioni kila mwenzi ambapo kwa sasa mapato yamepanda hadi kufikia milioni 80,000 kwa kila mwezi.

Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya viongozi, watumishi na wateja wa mamlaka hiyo ambao wamekuwa wakisisitizwa kulipa ankara zao za maji kwa wakati muafaka.

Kwa upande wao baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo, Philimon Ferdinand, pamoja na Joseph Evarist, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuguswa na mahitaji ya watumishi wa Mamlaka hiyo na kuamua kutoa fedha kwaajili ya ununuzi wa pikipiki tano kati ya 10 zinazotarajiwa.

"Kama ilivyo kwa watumishi wengine usafiri ni nyenzo njema ya kutufikisha haraka kwa wateja wetu hasa tunapokuwa tunafuatilia ubora wa maji kwenye makazi na taasisi mbalimbali za umma" amesema Frednand.




 

0/Post a Comment/Comments