Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepunguza kwa kiasi kikubwa ada za leseni kwa watoa huduma na wakusanya maudhui mtandaoni, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikikabili sekta hiyo na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidigitali.
Hatua hiyo imetangazwa leo Februari 12, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaofanyika kwa siku mbili.
Mwinjuma amesema Serikali iliagiza TCRA kufanya mapitio ya ada za leseni kufuatia malalamiko ya wadau waliokuwa wakilalamikia gharama kuwa kubwa na kikwazo kwa vijana wabunifu na wajasiriamali wa mitandao.
“Nafuraha kuwafahamisha kwamba ada za leseni kwa watoa maudhui mtandaoni zimepunguzwa kutoka Sh 500,000 hadi Sh 50,000, huku ada ya maombi ikiwa Sh 10,000 tu,” amesema Mwinjuma.
Ameongeza kuwa kwa wakusanya maudhui mtandaoni, ada ya leseni imepunguzwa kutoka Sh milioni moja hadi Sh 100,000, na ada ya maombi ni Sh 20,000.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, mapitio hayo yamekamilika rasmi na tayari yanaanza kutekelezwa, yakitarajiwa kuongeza urasimishaji wa shughuli za kidigitali na kupanua wigo wa ajira kwa vijana.
Amesema hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali na kuongeza mchango wake katika pato la taifa, huku ikifungua fursa zaidi kwa wabunifu wa maudhui, wanahabari wa mitandaoni na majukwaa ya kidigitali.
Katika hatua nyingine, Mwinjuma amesisitiza umuhimu wa kuboresha maslahi ya waandishi wa habari, akieleza kuwa mafunzo pekee hayawezi kuleta tija iwapo hawatakuwa na mikataba rasmi na malipo stahiki kwa wakati.
Amesema baadhi ya waandishi hawana mikataba ya ajira, huku wengine wakicheleweshewa malipo yao, jambo linalodhoofisha taaluma na ufanisi wao kazini.
“Naiagiza TCRA kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha utoaji wa leseni za utangazaji unaenda sambamba na uthibitisho wa mikataba ya ajira na malipo stahiki kwa wafanyakazi,” amesema.
Aidha, ameihakikishia sekta ya habari kuwa Serikali inaendelea kushughulikia madeni ya matangazo ya Serikali yanayodaiwa na vyombo vya habari ili yalipwe kwa wakati, hatua itakayosaidia kuimarisha mzunguko wa fedha katika sekta hiyo.
Hatua ya kupunguza ada za leseni inatajwa kuwa miongoni mwa maboresho makubwa katika sekta ya mawasiliano kwa mwaka 2026, ikitarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana katika ubunifu wa maudhui na kukuza tasnia ya kidigitali nchini.




Post a Comment