SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA WATEKELEZAJI WA MIRADI YA UTAFITI WA TABIANCHI


 ::::::::

Na Carlos Claudio, Dodoma.📍

Serikali imewataka watekelezaji wote wa miradi 39 ya utafiti wa tabianchi inayoratibiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa kwa ukaribu mkubwa na kila shilingi ya fedha za umma inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Wito huo umetolewa leo Februari 5, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, akimuwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Mapitio ya Maendeleo ya Utafiti wa Mpango wa Utafiti wa Tabianchi wa COSTECH.

Prof. Mushi amesema serikali ina matarajio makubwa kwa watafiti waliopata ufadhili huo, akieleza kuwa kati ya miradi 39, tayari miradi 34 imeanza kutekelezwa na mkutano huo unatarajiwa kupokea na kujadili matokeo ya awali ya tafiti kutoka kwenye miradi hiyo.

“Utafiti unaofadhiliwa kwa rasilimali za umma ni uwekezaji mkubwa. Kwenu nyie watafiti, huu ni deni kwa taifa. Tunategemea tafiti hizi zitoe majawabu ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzingatia mazingira halisi ya nchi yetu,” amesema Prof. Mushi.

Ameitaka COSTECH kuongeza ufanisi katika kuratibu programu hiyo kwa kuhakikisha fedha za utafiti zinasimamiwa vyema na matokeo ya tafiti yanaratibiwa na kuwasilishwa kwa wadau wote ikiwemo wizara husika, ili matokeo hayo yaweze kutumika katika kupanga sera, sheria na mipango ya maendeleo ya taifa.

Amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni janga linalogusa nyanja zote za maisha ikiwemo kilimo, afya, nishati, miundombinu, maliasili pamoja na mifumo ya kijamii na kiuchumi, hivyo tafiti zinazofanyika zinapaswa kuwa za vitendo na kulenga kutoa suluhisho endelevu.

“Tunahitaji ushahidi wa kisayansi ili kuunda sera na kanuni zitakazotuwezesha kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Tafiti hizi lazima ziwe na tija na ziendane na vipaumbele vya taifa,” amesema.

Aidha, amewataka watafiti kuwashirikisha wananchi, watendaji na watunga sera katika hatua mbalimbali za utafiti na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawasilishwa kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na kutumika bila vikwazo.

Akizungumzia dira ya maendeleo, Prof. Mushi amesema serikali inalenga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050yenye azma ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza kipato cha mwananchi hadi kufikia dola za Kimarekani 7,000, akisisitiza kuwa utafiti, sayansi, teknolojia na bunifu ni nguzo muhimu katika kufikia azma hiyo.

Katika hatua nyingine, ameishukuru serikali ya Sweden na Norway kwa msaada wa kifedha na kitaalamu katika kujenga uwezo wa utafiti nchini, akibainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kufungua milango ya ushirikiano na washirika wa maendeleo ili kuimarisha tafiti zenye tija kwa taifa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amewapongeza watafiti, wawezeshaji na washiriki wote kwa mchango wao katika kufanikisha mpango huo wa utafiti wa tabianchi.

Dkt. Nungu amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na mshikamano baina ya miradi mbalimbali ili kubaini maeneo ya kuongezeana nguvu (complementarity) na kuongeza athari chanya za tafiti hizo kwa jamii kwa ujumla.

Mkutano huo wa siku mbili unalenga kutathmini maendeleo ya tafiti zilizofadhiliwa, kubadilishana uzoefu na maarifa, kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza pamoja na kujenga kiungo madhubuti kati ya utafiti, sera na mipango ya maendeleo ya taifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.



0/Post a Comment/Comments