TAASISI UMO YAACHA ALAMA KATIKA HUDUMA ZA KIJAMII DODOMA

........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Taasisi ya Maendeleo na Uchumi (UMO) imeungana na wadau mbalimbali jijini Dodoma kutoa msaada na kuonesha matendo ya huruma kwa watoto yatima katika Kituo cha Rahman Orphanage Centre kilichopo Chang’ombe, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mwezi mtukufu wa Ramadhani sambamba na Kwaresma.

Akizungumza leo Februari 20, 2026 jijini Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri, mwakilishi wake Kassim Jonjolo aliipongeza UMO kwa juhudi zake za kusaidia wahitaji na kuhamasisha taasisi nyingine kuiga mfano huo. 

Alisisitiza kuwa matendo ya huruma hayapaswi kufanyika wakati wa vipindi maalum vya kiimani pekee, bali yawe sehemu ya maisha ya kila siku.

“Tunapenda kuipongeza UMO kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tunaendelea kuhamasisha taasisi nyingine kuungana nao, kwani vituo vya watoto yatima ni vingi hapa Dodoma na vinahitaji msaada wa kila mmoja wetu,” alisema Jonjolo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rahman Orphanage Centre, Rukia Hamisi Abdallah, aliishukuru UMO kwa kuandaa tukio hilo maalum na kusaidia watoto waliopo kituoni hapo. Alieleza kuwa kituo hicho kina watoto 120, wengi wao wakipatiwa mafunzo ya kujiajiri hususan katika sekta ya kilimo.

Hata hivyo, alitaja changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni pamoja na ukosefu wa usafiri wa kuwapeleka watoto shambani, upatikanaji wa nishati safi ya kupikia pamoja na bima ya afya kwa watoto.

Naye Katibu wa Chama cha Wazee Wanaume Mkoa wa Dodoma, Mchungaji George Nelson Nyandala, alisema tukio hilo ni kielelezo cha upendo na mshikamano katika jamii, akihimiza wananchi kuwajali yatima na wajane kama sehemu ya ibada.

Mwakilishi wa Wise Technology, Ibrahim Kassim Saidi, alieleza kuwa msaada huo hauoneshi ukamilifu wa watoa huduma bali ni ishara ya kujali na kuwapa matumaini watoto waliopoteza wazazi wao.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Ever Green and Community Development Initiative, Sheba Philip, aliishukuru UMO kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali na kueleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha jamii kuendeleza matendo ya huruma.

Aidha, Balozi wa Scan Code Tanzania, Bakari Kiwingu, aliipongeza UMO kwa kaulimbiu yao ya “Funga kwa amani na upendo,” akisema inaleta ujumbe mzito wa kudumisha amani na mshikamano huku ikiwahimiza wadau kujitoa kusaidia wenye uhitaji.

Akizungumza kwa niaba ya UMO, Katibu wa taasisi hiyo, Haruna Nchanjai, aliwashukuru wadau wote walioshiriki na kutoa wito kwa jamii kuendelea kuunga mkono juhudi hizo. Alibainisha kuwa baada ya tukio hilo, msafara utaendelea katika vituo vingine ikiwemo Miyuji.

Naye Mkuu wa Idara ya Afya wa UMO Taifa, Fadhir Magoyo, alitoa shukrani kwa wadau na vyombo vya habari kwa ushirikiano wao, huku akiiahidi Rahman Orphanage Centre kuwa UMO itaendelea kuitembelea na kusaidia kukabiliana na changamoto zilizopo.

UMO imepanga kuendeleza matukio kama hayo, likiwemo tukio jingine litakalofanyika Jumapili katika kituo cha masista Miyuji, ikiwa ni juhudi za kueneza upendo, huruma na mshikamano katika jamii.








 

0/Post a Comment/Comments