TAFORI YATAKIWA KUFANYA UTAFITI WA KINA KUTOKANA NA MAZAO YA NYUKI NA ASALI


........................

Na SaidI Lufune, Morogoro

Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imetakiwa kushirikiana ipasavyo na vyuo vilivyopo hapa nchini ili kufanya ufafiti wa kina juu ya mazao yatokanayo na nyuki ili taifa liendelee kunufaika na rasilimali hizo

Wito huo umetolewa Mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa hafla ya kufunga Bodi ya 12 ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo ambapo amesisitiza kuwa ipo haja ya kuendelea kufanya tafiti juu ya matumizi na faida za ziada zinazoweza kupatikana kutokana na matumizi mbadala ya mazao ya nyuki badala ya kujikita katika mazao yaliyozoeleka ya asali na nta.

“Andaeni mpango wa kwenda vyuoni, tusisubiri wanaotaka kufanya tafiti za misitu na nyuki ndio sisi tushirikiane nao, la hasha twendeni kutoa hamasa huko vyuoni, ili watu wafanye tafiti juu ya asali tulionayo, wafanye tafiti juu ya makundi yetu ya nyuki na pia kuwachukua wataalam waliopo vyuoni kufanya tafiti hizo ili waje kutusaidia katika taasisi yetu. Hivyo, fanyeni kazi kwa moyo mkunjufu na moyo mkubwa sana” amesisitiza Mhe. Chande

Katika hatua nyingine Mhe. Chande amesisitiza taasisi hiyo kufanya utafiti juu ya matumizi sahihi ya tiba ya nyuki itokanayo na sumu ya nyuki, maziwa ya nyuki na umuhimu wa asali na masega ya nyuki kwa afya ya mwanadamu ili kuongeza uzalishaji na uuzaji wa mazao hayo kwa wingi ikiwa ni malengo mahususi ya Serikali ya awamu ya sita ya kipindi cha pili cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

Aidha, ameipongeza TAFORI kwa kuendelea kufanya tafiti mbalimbali na kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kupitia makongamano na warsha ndani na nje ya nchi yanayochangia matokeo chanya katika tafiti zao.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Bernard Patrice Marcelline amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na taasisi zote zilizo chini ya Wizara, ikiwemo TAFORI kwa kuongeza idadi ya watumishi (watafiti) katika awamu hii ya serikali iliyopo madarakani

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Bodi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo inayomaliza muda wake, Prof. Verdiana Grace Masanja, amefafanuwa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya utendaji wa Bodi hiyo kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 hadi mwaka 2025/2026, taasisi imefanikiwa kukusanya shilingi billion 13.6 sawa na asilimia 67 ya makadrio, kushiriki kikamilifu katika kazi mbalimbali za kitaifa zinazolenga kuimarisha utendaji wa sekta na kuchangia maendeleo ya nchi kwa ujumla

Aidha, ameongeza kuwa Katika kipindi cha miaka mitatu TAFORI imetekeleza tafiti 17 ikiwemo tafiti 6 za kimkakati na 11 za kawaidi ikiwemo utafiti wa uvunaji wa miti aina ya misindao kuvunwa kuanzia miaka 18 na kuendelea kwa ajili ya matumizi ya mbao na umri wa kuanzia miaka 11 kwa ajili ya uzalishaji wa karatasi.







 

0/Post a Comment/Comments