TANZANIA IPO TAYARI KUSHIRIKI INDABA 2026

........

Dodoma

Imeelezwa kwamba Tanzania kupitia Wizara ya Madini na Taasisi zake pamoja na wadau mbalimbali waliopo katika mnyororo wa thamani madini zikiwemo taasisi za fedha kwa pamoja zipo tayari kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini wa Indaba unaotarajia kufanyika mjini Cape Town , Afrika Kusini kuanzia Februari 9 hadi 12, 2026.

Hayo yalielezwa Februari 2, 2026 na Naibu Katibu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo wakati wa kikao kilichojadili jinsi ushiriki wa Tanzania namna itakavyojinadi fursa zilizopo katika sekta ya madini pamoja na kuelezea kuhusu mageuzi mbalimbali yaliyofanyika.

Mbibo alisema kuwa, katika Mkutano huo , Tanzania inatarajia kujitangaza kama nchi yenye rasilimali nyingi za madini hususan kwenye madini ya mkakati na itashiriki mijadala na watu muhimu kuhusu uwekezaji , teknolojia na ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya madini.

Mbibo aliongeza kuwa, ushiriki wa Tanzania unaambatana na juhudi za serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuhakikisha kuwa sekta ya madini inawanufaisha wananchi kwa njia endelevu kupitia michakato ya kisasa na ushirikiano wa kimataifa.

Akielezea faida za ushiriki wa mkutano huo, Mbibo alieleza kuwa, baadhi ya faida za ushiriki ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali, kufungua wigo wa uwekezaji mpya wa sekta, kuonyesha fursa zilizopo katika rasilimali madini , kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana uzoefu na teknolojia za kisasa za uchimbaji kutoka mataifa mengine.

 _Mining Indaba_ ni jukwaa la kimataifa linalowaunganisha viongozi wa serikali , wawekezaji, makampuni ya madini na wataalam wa sekta ili kujadili fursa za uwekezaji , Sera na changamoto zinazoikabili sekta ya madini barani Afrika.

*Vision 2030: MadiniNiMaishaNaUtajiri*





 

0/Post a Comment/Comments