TANZANIA YAANDIKA HISTORIA MPYA: MRADI WA UMEME JUA KISHAPU WAKAMILIKA

:::::::::

Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya nishati baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa nishati ya jua ulioko Kishapu, mkoani Shinyanga mradi ambao ni mkubwa na wa kwanza wa aina yake nchini.

Akizungumza Februari 21, 2026 mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema kukamilika kwa mradi huo ni ushahidi wa dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika kwa Watanzania.

“Hii ni historia mpya imeandikwa kwa nchi yetu. Tangu tupate uhuru, hatujawahi kuwa na mradi mkubwa wa aina hii ya umeme wa jua. Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO imeandika historia, na leo mmeshuhudia hapa umeme ukizalishwa. Mpaka kufikia Machi 1, 2026 jumla ya Megawati 50 zitakuwa zimeunganishwa kwenye Gridi ya umeme ya Taifa,” alisisitiza Bw. Twange.

Bw. Twange ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa jumla ya Shilingi bilioni 118.6 kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), fedha zilizowezesha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amesema mradi huo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa eneo hilo, hasa kwa vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini na shughuli za kilimo.

“Mradi huu umeleta ajira kwa wananchi wetu na umefungua ukurasa mpya wa maendeleo. Umeme wa uhakika utaongeza tija katika sekta za madini na kilimo, na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Kishapu,” alisema Mhe. Masindi.

Naye Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme Kishapu, Mhandisi Mariana Mrosso, alieleza kuwa kituo hicho kitaimarisha uthabiti wa Gridi ya Taifa na kuboresha ubora wa upatikanaji wa umeme, hususan kwa wateja wa maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Umeme unaozalishwa hapa utaongeza uwezo wa uzalishaji kwenye Gridi ya Taifa na kuboresha ufanisi wa huduma kwa wateja wetu hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,” alifafanua Mhandisi Mrosso.

Imeelezwa kuwa ifikapo Machi 1, 2026, megawati zote 50 zitakuwa zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. 

Wakati huo huo, TANESCO ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo, itakayozalisha megawati 100 kwa gharama ya Shilingi bilioni 200.4 za kitanzania.

Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu unatajwa kuwa alama ya mabadiliko makubwa na hatua muhimu katika mwelekeo wa Tanzania kutumia matumizi ya nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa nishati zinazozalishwa nchini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa.








0/Post a Comment/Comments