Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda leo tarehe 18 Februari, 2026 katika ofisi za TRA Dar es salaam amezindua Bodi ya Usimamizi wa timu ya mpira wa miguu “TRA United Sports Club na kuitaka kuisimamia kikamilifu timu hiyo na kuifanya kuwa bora na tishio katika ligi za ndani na Kimataifa.
Pamoja na mambo mengine ameisisitiza kwenda kusimamia nidhamu ya timu ili kuifanya kuwa ya mfano dhidi ya vilabu vingine vinayoshiriki ligi mbalimbali nchini.
Amesema dhamira ya TRA kuianzisha timu hiyo mbali na kutoa burudani imelenga kupeleka ujumbe kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari jambo ambalo ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi wa nchi huku akitarajia matokeo chanya katika jambo hilo mara baada ya kuanzishwa kwa Bodi hiyo.
“Tumetengeneza timu kwa sababu dhamira yetu kubwa ni kwenda kufungamanisha wajibu wa TRA na ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi katika kuelewa umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, hivyo imani yangu nyinyi kama Bodi mtakwenda kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wananchi wanaliona suala la kulipa kodi kama jukumu lao na siyo vinginevyo” amesema Mwenda.
Amesema anatambua umuhimu wa suala la michezo nchini, hivyo kupitia timu hiyo pamoja na Bodi iliyoundwa matarajio yao ni kwenda kuwa kioo cha michezo nchini ikiwa ni pamoja na kutoa taswira kwa wachezaji hususani kutoka nje ya nchi kuchangia kodi kutoka katika mishahara wanayolipwa.
Kamishna Mwenda amesema ili kufikia malengo ya Dira ya Mwaka 2050, TRA ikiwa ndiyo injini katika dhamira ya kufikia kiwango cha pato la taifa, wana wajibu wa kuhakikisha wanatumia njia mbalimbali za ukusanyaji wa mapato ikiwemo kupitia sekta hiyo ya michezo, jambo analoamini kuwa kama bodi hiyo itaweza kutumia weledi wao kuisimamia timu hiyo wanaweza kufanikiwa kama ilivyo matarajio yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Timu ya ‘TRA UNITED’ Edmund Kawamala, pamoja na mambo mengine amempongeza Kamishna Mwenda kwa wazo lake la kuianzisha timu hiyo ambayo matarajio yake itakuwa kuwa moja ya timu tishio ya mpira wa miguu katika Bara la Afrika.
Amesema wakiwa kama Bodi, watahakikisha wanafanya kila linalowezekana kuiwezesha timu hiyo kupelekea ujumbe wa kulipa kodi kwa wananchi, wakiamini asilimia kubwa ya wananchi wanapenda michezo hivyo kupitia timu ya ‘TRA UNITED’ wananchi watapata elimu ya kodi.
Mbali na Mwenyekiti wake Edmund Kawamala, Bodi ya ‘TRA UNITED’ inaundwa na wajumbe wengine nane ambao ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Dkt. Wilfred Kidao, Mwenyekiti wa Taasisia ya Sekta Binafsi Tanzania Angelina Ngalula, Juma Kisongo, Kamna Shomari, Zahoro Salum, Paul Walalaze pamoja na Elikunda Mndeme ambao ni watumishi wa TRA huku nafasi ya mjumbe wa mwisho ikitarajiwa kujazwa wakati wowote.




Post a Comment