Mamlaka ya Mapato Tanzania (Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA) imezindua Kituo cha Huduma kwa Walipa Kodi Masaki jijini Dar es Salaam, hatua inayolenga kusogeza huduma karibu na wafanyabiashara na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Kituo hicho kinatarajiwa kurahisisha usajili, ulipaji na upatikanaji wa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara wa Masaki, Oysterbay na Msasani, maeneo yenye shughuli nyingi za kiuchumi na uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema uwepo wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha huduma na kupanua wigo wa walipa kodi katika eneo lenye wafanyabiashara wa kipato cha kati na juu.
Amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma, akieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha taratibu, kupunguza gharama kwa walipa kodi na kuongeza usawa wa kikodi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Kodi Kinondoni, Aziz Rajab Soka, amesema kituo hicho kinahudumia zaidi ya walipa kodi 6,700 na kinalenga kuongeza makusanyo ya kodi katika kipindi kilichosalia cha mwaka wa fedha. Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa vitengo maalum ikiwemo sekta ya majengo na upelelezi wa kodi kutaimarisha usimamizi wa mapato katika eneo hilo la kimkakati.








Post a Comment