Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imeongezewa muda wa siku 42 kuanzia Ijumaa, Februari 20, 2026, ili kukamilisha majukumu yake.
Tume hiyo iliyoundwa na kuzinduliwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ilianza kazi rasmi Novemba 20, 2025 kwa muda wa siku 90, uliotarajiwa kuhitimishwa Februari 20, 2026.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya tume, muda huo umeongezwa ili kuruhusu uchunguzi wa kina zaidi kuhusu matukio yaliyoripotiwa katika kipindi cha uchaguzi huo na baada yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyongeza hiyo inalenga kuipa tume nafasi ya kukusanya na kuchambua ushahidi wa ziada kuhusiana na matukio ya vurugu yaliyoripotiwa katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwamo maandamano yaliyosababisha vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa miundombinu ya serikali na mali za watu binafsi.
Kutokana na nyongeza hiyo, tume sasa inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kabla au ifikapo Aprili 3, 2026.
Katika matukio hayo, mamia ya watu walikamatwa na kufikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka mbalimbali, ikiwemo uhaini.
Baadhi ya washitakiwa hao wamepata msamaha wa rais, huku wengine wakiendelea na taratibu za kisheria.
Taarifa ya tume imeeleza kuwa kuongezwa kwa muda kutatoa fursa kwa wananchi wote wenye taarifa, ushahidi au maoni—waliopo ndani na nje ya nchi—kuwasilisha hoja zao, ili kuhakikisha kila upande unapata nafasi ya kusikilizwa kabla ya kukamilika kwa ripoti hiyo.

|
Post a Comment