Mkurugenzi
Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt Nkundwe Mwasaga wakati akitoa taarifa kuhusu kuanza
kwa utambuzi maalum wa kampuni changa za TEHAMA wakati alipozungumza na
wahabari leo tar 12/2/2026 jijini Dar es salaam
....................
Na MUSSA
KHALID
Tume
ya TEHAMA nchini (ICTC) imeanza zoezi la kusajili na kutambua kampuni changa za
TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa michakato ya upatikanaji mitaji na kuvutia mikopo
ya masharti nafuu inayotolewa na Serikali, taasisi za fedha, wawekezaji binafsi
na washirika wa maendeleo.
Pia
imeelezwa kuwa hadi kufikia mwezi Desemba 2025, zaidi ya kampuni changa 400
zilizo katika hatua mbalimbali za ukuaji na ubunifu, utoaji wa huduma
zilisajiliwa, huku kati ya hizo, kampuni 161 zimekidhi vigezo vya kuingia
katika programu mbalimbali za uendelezaji na uwezeshaji katika maeneo tofauti,
ikiwemo kitaalamu na rasilimali.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt Nkundwe Mwasaga wakati akitoa taarifa kuhusu kuanza kwa utambuzi maalum wa kampuni changa za TEHAMA ambapo kwa mujibu wa takwimu za Tume hiyo,zinaonyesha hadi kufikia Desemba 2025, zaidi ya vituo vya ubunifu 95 vimeanzishwa maeneo mbalimbali nchini.Aidha Dkt Nkundwe amesema kuwa Mpango huo wa utambuzi wa Kampuni changa za TEHAMA unalenga kufikia manufaa sita ikiwemo kuhamasisha ukuaji wa programu za ukuzaji bunifu za TEHAMA zinazotekelezwa na wadau mbalimbali, Kukuza ufanisi wa programu maalum ya kuzitangaza kampuni changa za TEHAMA kwa wawekezaji na masoko mbalimbali.
“Kuongeza ufanisi wa uwezeshaji wa kampuni changa za TEHAMA kufikia vigezo vya nafuu ya uwekezaji, Ugavi na manunuzi ya umma, nafuu ya leseni za udhibiti chini ya mamlaka mbalimbali inayotolewa na Serikali kupitia taasisi mbalimbali kwa mujibu wa sheria, Kukuza ufanisi wa programu maalum ya kuzitangaza kampuni changa za TEHAMA kwa wawekezaji na masoko mbalimbali mikutano mikubwa ya kibiashara na kiserikali inayofanyika ndani na nje ya nchi na kupitia makubaliano ya kidiplomasia ya uwili (bilateral) au uwingi (multilateral) baina ya Tanzania na nchi Nyingine”amesema
Pia Dkt Nkundwe amesema mpango huo uitawezesha ICTC kutambua changamoto zinazozikabili kampuni hizo na kushirikiana na wadau mbalimbali kuanzisha jitihada za ujenzi wa miundombinu wezeshi, kutafuta na kutoa mafunzo ya kitaalamu ya biashara na ujasiriamali kwa kampuni zilizo katika hatua ya awali ya ukuaji (early stage), pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni zilizo katika hatua ya ukuaji (growth stage).
Mkurugenzi huyo amezitaka kampuni changa kujisajili na kupata utambuzi maalum unaotolewa na Tume ya TEHAMA, ili iweze kutambuliwa na kuingizwa katika programu mbalimbali za uwezeshaji kwani mchakato huo hauna gharama yoyote kwa kampuni changa za TEHAMA.
Dk Nkundwe amesema Usajili kwa ajili ya utambuzi maalum kwa kampuni changa za TEHAMA unafanyika kwenye mfumo wa kielektroniki kupitia kikoa https://tanzaniastartups.ictc.go.tz ulio chini ya Tume ya TEHAMA na Orodha ya Kampuni zote changa za TEHAMA zitakuwa zikipatikana wowote katika tovuti ya Tume ya TEHAMA www.ictc.go.tz.
Post a Comment