Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imezindua mpango kabambe wa kurasimisha ujuzi wa vijana na wananchi 80,000 nchini kupitia programu maalum inayojulikana kama “Mama Samia”, hatua inayolenga kuthibitisha rasmi ujuzi wa mafundi na wataalamu waliopata maarifa nje ya mfumo rasmi wa mafunzo.
Akizungumza Februari 16, 2026 jijini Dodoma katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Mzee Kasore, amesema mpango huo utatoa vyeti vinavyotambua na kuthibitisha ujuzi wa wananchi wenye taaluma mbalimbali.
Amesema mafundi wengi wa magari, umeme wa majumbani, ujenzi na taaluma nyingine za mitaani wana ujuzi mkubwa lakini hawana vyeti rasmi, hali inayowakosesha fursa za ajira na zabuni. Kupitia mpango wa Urasimishaji Ujuzi (Recognition of Prior Learning – RPL), mafundi 25,523 tayari wamerasimishiwa ujuzi wao hadi Januari 2026.
“Kwa mwaka wa fedha 2025/2026 tumelenga kurasimisha mafundi 30,000, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mama Samia inayokusudia kufikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027,” amesema CPA Kasore.
Ameeleza kuwa vyeti hivyo vitawasaidia wahitimu kushiriki kwenye tenda mbalimbali, kupata ajira rasmi na kujiimarisha kiuchumi.
Katika hatua nyingine, CPA Kasore amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo mkubwa katika kuendeleza elimu ya ufundi stadi kama nguzo muhimu ya ajira, uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Leo hatuzungumzii nadharia. Tunazungumzia maisha ya vijana kubadilika, ajira kuundwa na uchumi kujengwa kwa mikono ya Watanzania wenye ujuzi,” amesema.
Kwa sasa, VETA ina vyuo 80 vinavyohudumia zaidi ya wanafunzi 86,000 kwa mwaka. Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo katika wilaya 64 pamoja na chuo kimoja mkoani Songwe, ikiwa na lengo la kuhakikisha kila wilaya inakuwa na angalau chuo kimoja cha VETA. Ifikapo mwaka 2027, idadi ya vyuo inatarajiwa kufikia 152 na kuongeza udahili hadi wanafunzi 250,000 kwa mwaka.
Katika kurahisisha upatikanaji wa mafunzo, VETA imeondoa mtihani wa mchujo (aptitude test), hatua iliyowezesha waombaji wote 18,875 wa mwaka huu kuchaguliwa kujiunga na mafunzo. Pia, wahitimu wa elimu ya juu wanaojiunga na VETA wameondolewa baadhi ya masomo waliyokwisha soma ili kuhitimu kwa muda mfupi zaidi.
Aidha, wanafunzi 195 wenye ulemavu wamefadhiliwa kikamilifu mafunzo yao ya muda mrefu mwaka huu, huku taasisi hiyo ikianzisha mafunzo ya jioni (Evening Session) kwa wananchi wanaofanya kazi au wenye majukumu ya asubuhi.
Katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, VETA inaendesha mfumo wa mafunzo kwa njia ya kielektroni ujulikanao kama VSOMO, unaowezesha wanafunzi kujifunza nadharia kwa simu au kompyuta kabla ya kuendelea na mafunzo ya vitendo.
Zaidi ya wanafunzi 500 tayari wamehitimu kupitia mfumo huo katika fani mbalimbali zikiwemo umeme, ufundi magari, upishi, urembo na ujasiriamali.
CPA Kasore amesisitiza kuwa dunia ya sasa inahitaji uwezo wa kufanya kazi kuliko vyeti pekee.
“Ujuzi ni mtaji, ujuzi ni ajira, ujuzi ni kujitegemea na ujuzi ni heshima,” amesisitiza.



Post a Comment