WATUMISHI SEKTA YA AFYA KWIMBA WAPATA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI GESI YA KUPIKIA


::::::::

Na Mwandishi Wetu,Kwimba

WATUMISHI wote wa idara ya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia sambamba ba kuelezea kwa kina madhara yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa kiafya.

Mafunzo hayo yametolewa na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania ambapo lengo kuu ni kuiwezesha kada hiyo ya sekta ya afya kuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi na kisha watumishi hao wawe mabalozi kwa wananchi wengine wakiwemo wagonjwa.

Akizungumza Februari 27,2027 wakati wa utolewaji wa mafunzo hayo kwa watumishi wa sekta ya afya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza Mkuu wa Mafunzo wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba amesema hatua hiyo ni katika muendelezo ule ule wa jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia 

Tumeamua kuchukua kundi la idara ya afya katika Wilaya hiyo.

“Oryx Gas tumeamua kutoa mafunzo haya kwa watumishi wa afya wa Wilaya ya Kwimba kwasababu tunajua wananchi wanapopata matatizo ya kiafya wanakuja hospitali kwahiyo wale ndio wanakuwa watu wa kwanza kukutana na wananchi wenye matatizo.

“Kwahiyo tumeamua kuwapa mafunzo ya ndani kabisa kuhusu matumizi sahihi ya gesi,usalama na kila kitu kuanzia athari ya kimazingira pamoja na athari za kiafya.Kwahiyo tumekuwa na kundi kubwa la watumishi wote wa sekta ya afya  zaidi ya 267 wakiwemo wa  Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wamepata mafunzo haya kwa siku  mbili kuhusu nishati safi ya kupikia 

“Tunafurahi mwitikio ni mkubwa na mafunzo haya ni mwanzo tu kwani tutakwenda katika taasisi zote,shule mbalimbali na kila jukwaa tutaweza kufika ili sasa muendelezo mzima wa matumizi ya nishati safi uweze kufikia watu wote”

Aidha Ndomba ametoa shukrani uongozi mzima wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, DMO pamoja na Mganga Mfawidhi kwa kuwapatia  nafasi ya kukutana na Madaktari na wauguzi kuwapa elimu ya gesi ambayo watu wengi hawaijui.

“Tumegundua kuna haja ya kupeleka elimu hii kwao ili wawe mabalozi wanapokutana na wananchi,wagonjwa hasa wamama wanaokuja hospitali kwa matatizo mbalimbali na kuwafafanulia kwamba matumizi ya nishati ndio jambo muhimu na itasaidia kupunguza matatizo mengi yanayotokea kutokana na matumizi ya kuni na mkaa,”amesema Ndomba.

Kwa upande wao watumishi wa sekta ya afya katika Wilaya hiyo wameishukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo ambapo wengine wamekiri wamekuwa wakitumia gesi ya kupikia kwa muda mrefu lakini hawakuwa wanajua faida na hasara zake lakini kupitia mafunzo hayo sasa watakuwa mabalozi kwa wengine.

Kwa upande wake  Christian Mvula amesema ambaye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba amesema wanashukuru Oryx kwa kuwapatia mafunzo ya matumizi sahihi ya gesi sambamba na kuachana na mkaa na kuni na kuingia katika matumizi ya gesi.

“Ukweli tumepata elimu sahihi ya kutumia gesi ya kupikia kama nishati ya kupikia majumbani na sisi watumishi tunafufahi kupata huduma hiyo na kimsingi tulikuwa tunateseka kutumia kuni na mkaa ambayo wakati mwingine ni ngumu kupatikana hasa kipindi hiki cha mvua.

“Lakini baada ya mafunzo haya tumeelewa matumizi ya gesi iliyosalama kama nishati ya kupikia na kwetu imekuwa nafuu kwani awali tulikuwa na uelewa tofauti, kulikuwa na nadharia nyingi mtaani kuhusu gesi ikiwemo usalama na gharama.Pia tumeelimishwa jinsi ya kutunza gesi ,kuikagua kila siku ili kuepusha changamoto na tumeelimishwa kuhusu madhara ya kuni na mkaa.”

Wakati huo huo Ofisa Muuguzi Salome Malale amesema ametumia gesi kwa miaka 15 lakini hakujua faida na hasara za gesi na yeye kama muuguzi kuna changamoto nyingi zimetokea kwa mfano jamii nyingi zinatumia kuni na mkaa.

“Ninavyojua walikuwa wanapata matatizo ya mapafu wengine macho na walikuwa wanakuja kutibiwa hospitalini, sasa kwa elimu ambayo nimeipata naweza kutoa elimu kwa jamii kutumia gesi na tuachane kutumia kuni au mkaa.

Kwa upande wake Robert Mayombya ambaye ni mtumishi wa hospitali ya Wilaya ya Kwimba amesema amefurahi kupata elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.”Nimejifunza matumizi mazuri ya gesi badala ya kutumia kuni na mkaa na nina imani nitatoa elimu kuanzia familia hadi majirani ili waachane na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake tutumie gesi.”








 

0/Post a Comment/Comments