Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wananchi wa Mtaa wa Mazengo, Kata ya Zuzu jijini Dodoma, wameiomba Serikali kuingilia kati na kusitisha mara moja shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi zinazoendelea katika eneo lao, wakieleza kuwa zinahatarisha maisha yao na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Ombi hilo lilitolewa wakati wa ziara ya Diwani wa Kata ya Zuzu, Mhe. Jenesta Malingo, aliyefika kusikiliza kero za wananchi na kutoa mrejesho wa hatua zilizochukuliwa na uongozi wa kata kuhusu chimbo hilo lenye utata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walieleza kuwa wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na kina kikubwa cha chimbo hilo lililopo karibu na makazi yao pamoja na taarifa za watu waliopoteza maisha katika eneo hilo.
“Tunaiomba Serikali isitishe uchimbaji huu mara moja, maisha yetu yako hatarini. Hili shimo ni kubwa na likijaa maji linaweza kusababisha maafa makubwa,” alisema mmoja wa wananchi katika mkutano huo.
Wananchi hao waliongeza kuwa pamoja na baadhi ya vijana kunufaika na ajira katika chimbo hilo, usalama wao unapaswa kupewa kipaumbele zaidi kuliko maslahi ya kiuchumi.
Akijibu hoja hizo, Diwani wa kata ya Zuzu Mhe. Jenesta Malingo amesema uongozi wa kata ulishachukua hatua mbalimbali kushughulikia suala hilo, ikiwa ni pamoja na kufanya ziara katika eneo la chimbo na kubaini hatari zilizopo.
Alisema baada ya tathmini hiyo, walikubaliana kupendekeza mwekezaji kuhamishiwa eneo jingine nje ya makazi ya watu ili kulinda maisha ya wananchi.
“Sisi kama kata hatuna mamlaka ya kutoa au kufuta leseni, lakini tuna wajibu wa kushauri. Tulipeleka mapendekezo yetu kwa mamlaka husika na Mkurugenzi wa Jiji alishatoa maelekezo ya kufutwa kwa leseni ya uchimbaji katika eneo hili,” alisema Malingo.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na maelekezo hayo, bado mamlaka za madini zimemruhusu mwekezaji kuendelea na shughuli za uchimbaji, jambo ambalo limezua mkanganyiko na malalamiko zaidi kutoka kwa wananchi.
“Ni kweli kuna changamoto ya utekelezaji wa maamuzi. Wakati sisi na uongozi wa jiji tumeonesha hatari iliyopo na kuomba shughuli zisitishwe, bado mwekezaji ameendelea na kazi baada ya kuruhusiwa na mamlaka za madini,” alifafanua.
Diwani huyo alisisitiza kuwa ataendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha usalama wa wananchi unalindwa, huku akitoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka na za kudumu.
Katika hatua nyingine, aliwahamasisha vijana wanaotegemea kipato kutoka kwenye chimbo hilo kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya serikali na kuanzisha shughuli mbadala za kiuchumi.
Ziara hiyo pia ilitoa fursa kwa wananchi kuwasilisha kero nyingine, ikiwemo changamoto ya umeme, ajira na miundombinu, ambapo diwani huyo aliahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Wananchi wa Mazengo walisisitiza kuwa wanahitaji hatua za haraka zaidi kutoka serikalini ili kuondoa hatari inayotokana na uchimbaji huo, wakiamini kuwa usalama wao ni wa msingi kuliko shughuli hizo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mazengo walieleza kufurahishwa na ziara hiyo wakisema imewapa fursa ya kueleza kero zao na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali.
Bi. Christina Mkobalo alisema ziara hiyo imewasaidia wananchi kufungua mioyo yao na kueleza changamoto zilizokuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu.
Naye Pascal Manyilika alisema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa vyema masuala ya maendeleo pamoja na namna ya kuwasilisha kero zao kwa viongozi.
Diwani huyo aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo ili kushiriki kikamilifu katika mijadala ya maendeleo na kuchangia mawazo yatakayosaidia kuboresha ustawi wa Kata ya Zuzu.





Post a Comment