Na. Sixmund Begashe, Babati
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Serikali kwa ujenzi wa lango la Mamire (Geti) la kuwawezesha watalii wa ndani na nje kuingia katika Hifadhi ya Taifa Tarangire kwa kupitia Babati Mkoani Manyara.
Akizungumza baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb), amesema kukamilika kwa lango hilo kuitafanya hifadhi hiyo kuwa na malango matano ambayo yatasaidia kuchechemua uchumi wa Wananchi wa Babati na Taifa kwa ujumla
Ameongeza kuwa ujenzi wa lango hilo ni jitihada na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwamba zinapaswa kuungwa mkono ili kuendeleza utali nchini.
Pamoja na kuipongeza Wizara hiyo, Mhe. Mnzava ametoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia vyema ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) ameihakikishia Kamati hiyo kuwa ofisi yake itasimamia vyema maoni yote yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo.
Aidha, Mhe. Chande ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za ujenzi wa lango hilo, hususan za ubunifu wa mazao ya utalii wa kiutamaduni kwa wageni watakao pitia Babati kuingia Hifadhi ya Taifa Tarangire.









Post a Comment