MBUNGE CHATO AWANANGA WALIOSHANGILIA KUKAMATWA NA TAKUKURU

.........

CHATO

MBUNGE wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe, amewananga baadhi ya wananchi walioshangilia kukamatwa kwake na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na rushwa(Takukuru) kisha kufikishwa mahakamani kwa makosa ya rushwa.

Hata hivyo amesema yupo tayali kuendelea kupambana na kesi hiyo wala hawezi kutetereshwa na nia ovu ya baadhi ya watu wenye lengo la kumdhoofisha.

"Nimesikia upo mpango wa kunifunga eti miezi sita na siku 3 ili nipoteze Ubunge wangu, niwahakikishie wenye mpango huo hamtaniweza, lazima nipige miaka yangu mitano, kama mnampango huo mjipange baada ya miaka mitano ijayo"amesema Magembe.

Mbali na hilo, amesema utendaji mbovu wa baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Chato ulisababisha yeye kususia kushiriki kwenye uzinduzi wa radio ya "Chato Fm" ambayo inamilikiwa na halmashauri hiyo kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya gharama za uanzishwaji wa mradi huo.

Alikuwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye stendi ya zamani ya Chato mjini ambapo pamoja na mambo mengine amesema hawezi kukubali kufanya kazi na viongozi wasiokuwa na uchungu na Jimbo hilo.

Kabla ya kupokea kero mbalimbali za wananchi Magembe amesema kukamatwa kwake na Takukuru kisha kufikishwa mahakamani kumetokana na baadhi ya watu kumfanyia hiyana ili kumvunja moyo wa kuwatumikia wananchi wake.

Amesema kutokana na yeye kutoyumbishwa katika misimamo yake yupo tayali kuendelea kuwekwa mahabusu mara kwa mara na kwamba kazi kubwa ya wananchi ni kuendelea kumwombea dua na sala kwa kuwa amedhamiria kupambania maendeleo.

Hata hivyo amewatuhumu viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Chato, kumnyima ushirikiano wa kuwatumikia wananchi jambo ambalo limekuwa likimkatisha tamaa kuwafikia wananchi hao.

Kadhalika amewataka kutambua kuwa Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025 umeshamalizika na kwamba viongozi waliostahili wameshapatikana, hivyo ni wakati wa kupewa ushirikiano kwa manufaa ya wananchi.

                         Mwisho.


 

0/Post a Comment/Comments