MBUNGE WA MBARALI AWEKA MIKAKATI YA MAENDELEO KWA KUSIKILIZA WANANCHI


*****

Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo, amesema ataongoza jimbo hilo kwa kusikiliza wananchi na kuwasemea katika vyombo vya maamuzi ili kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

Akizungumza katika mahojiano na mwandishi, Ndingo alisema katika kipindi chake cha ubunge atakuwa daraja kati ya wananchi na Serikali kwa kuhakikisha  maoni, ushauri na mapendekezo yao yanapelekwa kwenye hatua za utekelezaji.

Alisema dhamira yake ni kufuatilia kwa karibu masuala muhimu ya maendeleo ya jimbo hilo, hususan kwa kuibua hoja na kuzifikisha bungeni ili zipatiwe ufumbuzi kwa manufaa ya wananchi wa Mbarali.

“Ubunge wangu huu nitakuwa daraja la wananchi wangu, kuwasikiliza kwa yale wanayonishauri na kuyapeleka katika hatua za utekelezaji huku nikifuatilia zaidi,” alisema Ndingo.

Mbunge huyo alisema Mbarali ni miongoni mwa maeneo yanayotegemea zaidi uchumi wa kilimo, hasa zao la mpunga, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Alieleza kuwa kipindi cha masika kimesababisha baadhi ya barabara kuharibika, jambo ambalo limeathiri mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali ya jimbo hilo. Hata hivyo, alisema matarajio ni kwamba Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) utaanza kazi ya kurekebisha miundombinu hiyo mara baada ya mvua kupungua.

Ndingo pia alisema amejiwekea dhamira ya kutumia nafasi yake katika Bunge lijalo kutoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya wananchi wa Mbarali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati ya kuwahudumia wananchi, na kwamba yeye kama mbunge anao wajibu wa kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa ushauri na mchango unaolenga kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.

Kwa upande mwingine, aliwataka wananchi wa Mbarali kuwa na umoja na kuzungumza lugha moja yenye lengo la kujenga jimbo lao kwa pamoja, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji mshikamano na ushirikiano kutoka kwa kila mmoja.

Alisema kwa ushirikiano huo, Mbarali inaweza kufikia maendeleo yanayoonekana na kuwanufaisha wananchi wake katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
 

0/Post a Comment/Comments