Mfumo utabiri kiasi cha maji nyenzo ya takwimu sahihi za maji

........

Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Maji ni raslimali ya asili ambayo inatumika katika maeneo mengi muhimu yanayochagiza maendeleo. Upo umuhimu wa wananchi kuelimishwa ili kuielewa sekta ya maji kwa mapana badala ya kuona maji kama huduma ya kijamii pekee kwa shughuli za nyumbani kama kupikia, kufulia na kuogea. Maji ni zaidi ya matumizi hayo yaliyozoeleka kwa baadhi ya watu. Kwa nchi yetu yenye vyanzo vingi vya maji lakini wakati huo huo ina idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi zinazohitaji maji, takwimu sahihi za maji zinapaswa kuwepo ili tusiwe watu wa kubahatisha kuelewa kiasi cha maji tulichonacho nchini na mahitaji halisi ya maji kufanikisha mipango na shughuli mbalimbali za maendeleo. Bila takwimu sahihi tutakwama na hatutakuwa na uhakika wa kufanikisha mambo yetu kama nchi.

Katika masuala ambayo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesisitiza kuyasimamia kikamilifu na kuyapa kipaumbele ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli mbalimbali za maji ili kuongeza kasi ya utendajikazi na ufanisi. Wizara ya Maji imekuja na teknolojia ya kisasa ya mfumo wa utabiri wa kiasi cha maji ya mito. Mfumo huu ulizinduliwa Machi 22, 2026, na Makamu wa Rais Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, katika Bwawa la Mindu Morogoro Mjini ikiwa ni kilele cha Wiki ya Maji Tanzania na Siku ya Maji Duniani. Mfumo huo ni teknolojia ya aina yake iliyokuja wakati sahihi.

Teknolojia hii ni muhimu hasa kipindi hiki ambacho mahitaji ya maji yameongezeka lakini pia kipindi hiki cha utekelezaji wa mradi wa Gridi ya Taifa ya Maji ikiwa ni agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunakuwa na Gridi ya Taifa ya Maji ambayo itapokea maji kutoka vyanzo mbalimbali vya maji na kuyatumia maji hayo kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo endelevu. Mfumo wa utabiri wa kiasi cha maji ya mito unatoa taarifa ya kiwango cha maji tulichonacho kama nchi. 

Hii itatupa picha kama kiasi kilichopo kinakidhi mahitaji ya Taifa au la. Na kama hakikidhi mahitaji, basi kama Taifa tutachukua hatua stahiki kuhakikisha tunaongeza kiwango cha maji ili kuepusha kukwamisha shughuli za kimaendeleo zinazohitaji maji kwa kisingizio cha upungufu wa maji. Ni muhimu kupunguza visingizio katika jitihada za maendeleo. Makamu wa Rais Dk. Nchimbi akisisitiza suala la usambazaji wa maji kwa wananchi kwani wanawake ni wahanga wakubwa. " Wanawake wana mchango wa kipekee shida ama Raha katika maji ni zaidi ya asilimia 60 wamekuwa watu wa maji usiku na mchana katika changamoto ya Maji na kutunza familia," amesema.

Kimsingi, mfumo wa utabiri wa kiasi cha maji ya mito nchini ni dira yetu kamili ya kuweka mikakati ya kujitosheleza kwa mahitaji ya maji. Kupitia mfumo huu, tutapata takwimu za kiwango cha maji kilichopo na kuongeza hamasa ya utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji ili tuendelee kuvuna maji zaidi kwa maendeleo ya sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, uvuvi, miundombinu, madini na shughuli nyingine muhimu za kijamii. Mikakati mizuri ya maendeleo iliyopo inategemea sana uwepo wa raslimalimaji.

Mathalani, shughuli za ujenzi kama barabara na madaraja zinahitaji maji. Kilimo cha uhakika kinategemea sana maji kwa ajili ya umwagiliaji. Uvuvi na mifugo inahitaji maji. Viwanda vinahitaji maji. Shule na hospitali zinahitajika maji. Uzalishaji umeme pia unahitaji maji. Maji yanagusa sekta nyingi za maendeleo. Kwa maneno mengine, kufanikiwa kwa mipango mizuri ya maendeleo kunategemea sana uwepo wa maji ya uhakika. Tunawezaje kuwa na uhakika wa kutumia maji katika shughuli za maendeleo kama hatuna taarifa za uhakika? Ndiyo maana mfumo wa utabiri wa kiasi cha maji ya mito umezinduliwa ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za maji.

Kufanikiwa kwa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 kunategemea sana upatikanaji wa maji safi, salama na yenye kutosheleza. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Dk. Nchimbi, inakadiriwa Tanzania kufikisha watu millioni 118 ifikapo mwaka 2050. Serikali itawezaje kuwahudumia wananchi wote hao na kutekeleza shughuli za maendeleo zinazohitaji maji pasipo kuwa na taarifa sahihi za hali ya upatikanaji wa maji nchini? Mfumo wa utabiri wa kiasi cha maji umekuja kujibu suala hilo. Pamoja na yote mazuri kuhusu sekta ya maji, suala la utunzaji na ulinzi wa vyanzo vya maji ni muhimu sana. 


Uhakika wa ulinzi na usalama wa vyanzo vya maji unachagiza kufikiwa kwa mipango ya maendeleo inayohitaji uwepo wa maji. Ni vyema wananchi tukawa mabalozi wazuri wa kutunza vyanzo vya maji na kutoa taarifu tunapoona upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali ili hatua muhimu zichukuliwe kutatua changamoto hiyo. Sote tunategemea maji katika shughuli zetu za kila siku, tutakuwa wageni wa nani kama tutaharibu vyanzo vya maji? Ujio wa mfumo wa utabiri wa kiasi cha maji iwe ni hamasa ya kuongeza uzalishaji wa maji ili tuwe na maji ya ziara yenye kutosheleza mahitaji yote ya nchi na kuwa na ya ziada kwa maendeleo ya uhakika.

Maoni: 0620 800462.







 

0/Post a Comment/Comments