Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari bin Zubeir, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuzingatia uaminifu, uadilifu na weledi wanapotekeleza majukumu yao ili kulinda maslahi ya taifa.
Akizungumza katika iftari maalum iliyoandaliwa na Kamishna Mkuu wa TRA jijini Dar es Salaam, Mufti Zubeir aliwapongeza viongozi na wafanyakazi wa mamlaka hiyo kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kukusanya mapato ya serikali.
Alisema maadili ya uaminifu na uadilifu ni msingi muhimu katika utendaji wa kazi, akibainisha kuwa hata katika mafundisho ya dini, mtu anatakiwa kufanya kazi yake kwa weledi na ubora kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mufti Zubeir pia aliwataka waumini kutumia vyema siku zilizobaki za kumi la mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuongeza ibada, dua na kuliombea taifa liendelee kuwa na amani na ustawi.
Aidha, aliwasihi kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake ili waendelee kuiongoza nchi kwa mafanikio na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema taasisi hiyo itaendelea kuhamasisha wananchi kufuata sheria za kodi kwa hiari na kulipa kodi kwa uadilifu kama sehemu ya uwajibikaji kwa taifa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ameipongeza TRA kwa juhudi zake za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kuwasisitiza wananchi kudai na kutoa risiti, akisema kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi.
.jpg)













Post a Comment