Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imegawa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 769 kwa shule za msingi na sekondari 19 zilizopo katika mikoa tisa nchini, ikiwemo Kusini Unguja (Zanzibar), Dodoma, Iringa, Ruvuma, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo iliyofanyika jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kisasa.
Alisema matumizi ya vifaa hivyo yataongeza uelewa kwa wanafunzi kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo na kuona, hasa katika masomo ya sayansi na teknolojia. Aidha, alieleza kuwa walimu watanufaika kwa kutumia mbinu bunifu za ufundishaji, kuandaa maudhui kwa ufanisi na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa urahisi kupitia mifumo ya kidijitali.
“Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kama yalivyoainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) pamoja na mitaala iliyoboreshwa, kwa lengo la kuboresha ubora wa elimu na kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye,” alisema Ameir.
Alitaja baadhi ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuwa ni pamoja na utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kuanzishwa kwa mkondo wa elimu ya amali unaolenga kuwapatia wanafunzi stadi za ufundi na ujasiriamali, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika ufundishaji, ujifunzaji na usimamizi wa elimu.
Aidha, aliongeza kuwa Serikali imeandaa na kuanza kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu, sambamba na miongozo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa matumizi ya TEHAMA katika shule na vyuo vya ualimu pamoja na mwongozo wa matumizi ya Akili Unde (AI) katika elimu.
Kwa upande mwingine, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imeanzisha madarasa janja matano na kufunga mbao janja 422 katika shule za sekondari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya ujifunzaji nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha elimu kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21, hususan kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Alisema ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu pamoja na mkakati wa TEHAMA katika sekta hiyo, na ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata nyenzo bora za kufundishia na kujifunzia.






Post a Comment