Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga kunatarajiwa kuchochea shughuli za kibiashara na uwekezaji, hatua itakayosaidia kuimarisha muunganiko wa kiuchumi kati ya mkoa huo na mikoa jirani.
Ulega ametoa kauli hiyo mkoani Shinyanga mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kueleza kuridhishwa na utekelezaji wake uliofikia asilimia 94.9.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wenye lengo la kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Ulega amemuelekeza mkandarasi CHICO kuongeza nguvu kazi ya watumishi pamoja na vitendea kazi ili kukamilisha ujenzi wa jengo la abiria kwa wakati uliopangwa kwenye mkataba.
“Hakikisheni ndani ya siku 45 zilizobaki mnafanya kazi usiku na mchana ili mkamilishe jengo la abiria na kiwanja hiki kiweze kutoa huduma iliyokusudiwa,” amesisitiza Ulega.
Waziri huyo pia ameipongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Shinyanga pamoja na mkandarasi CHICO kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa mita 2,200 ambayo itawezesha kuhudumia kwa usalama ndege za kibiashara aina ya Bombardier Dash 8 Q400.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, alisema mradi huo ulianza Aprili 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026 ambapo unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 44.8.
Amefafanua kuwa mradi huo umehusisha kazi mbalimbali za ujenzi ikiwemo barabara ya kuingia kiwanjani, barabara ya mzunguko ndani ya uwanja, maegesho ya magari, jengo la abiria linalojumuisha mnara wa kuongozea ndege na barabara ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa mita 2,200 na upana wa mita 30.





Post a Comment