TAKUKURU YAONGEZA NGUVU SEKTA YA AFYA TEMEKE

            ******
Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesisitiza kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii sambamba na jukumu lake la msingi la kupambana na rushwa, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, alisema msaada huo unalenga kusaidia juhudi za kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga, hasa wanaozaliwa kabla ya muda.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila.

Alifafanua kuwa pamoja na mapambano dhidi ya rushwa, taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa umma pamoja na kufanya tafiti na uchambuzi wa mifumo ili kuzuia mianya ya vitendo vya rushwa.

Chalamila alieleza kuwa bado kuna changamoto kubwa ya vifo vya watoto wachanga, hususan njiti, hali inayohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kupunguza tatizo hilo. Aliongeza kuwa TAKUKURU itaendelea kushirikiana na sekta ya afya kuhakikisha huduma zinaboreshwa na maisha ya watoto yanaokolewa.

Katika hatua nyingine, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya afya, hususan katika huduma za mama na mtoto, hatua iliyochangia kutambuliwa kwake katika ngazi ya bara la Afrika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alisema msaada huo umewadia wakati muafaka kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za watoto wachanga hospitalini hapo.

Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na mzigo mkubwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum ambazo zina gharama kubwa, hivyo msaada kutoka kwa wadau ni muhimu katika kusaidia kuokoa maisha ya watoto.

Mapunda pia alipongeza ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na ofisi ya wilaya, akieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele si tu katika kupambana na rushwa bali pia kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii, hali iliyoongeza imani ya wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda.

Naye Daktari Bingwa wa Watoto, Dk. Irene Karamaga, aliyewakilisha uongozi wa Idara ya Watoto katika hospitali hiyo, alisema kuna ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa kabla ya muda, jambo linaloongeza uhitaji wa huduma maalum.

Alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha karibu nusu ya watoto wanaolazwa hospitalini hapo ni njiti, huku zaidi ya asilimia 40 ya watoto wachanga wanaopokelewa wakiwa wamezaliwa kabla ya muda.

Dk. Karamaga alieleza kuwa licha ya jitihada za wataalamu wa afya, bado kuna changamoto ya uhaba wa vifaa tiba na wataalamu bingwa, hali inayochangia hatari ya vifo kwa watoto hao.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwemo TAKUKURU, una mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya na kuongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya watoto wachanga.











0/Post a Comment/Comments